The House of Favourite Newspapers

Watatu Waandaliwa Mikataba Mipya Simba

0

SIMBA ipo kwenye mipango ya mwisho kukamilisha usajili wa viungo wake wawili, Sharraf Eldin Shiboub, Mzamiru Yassin na beki wa kati Muivory Coast, Pascal Serge Wawa.

 

Wachezaji hao ni kati ya wale tisa wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu, wengine ni Hassan Dilunga, Yusuf Mlipili, Deo Kanda, Clatous Chama pamoja na Paul Bukaba na Mohammed Ibrahim ‘Mo’ wanaokipiga kwa mkopo Namungo FC ya Ruangwa, Lindi.

 

Nyota hao kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ni wachezaji wanaoruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayowahitaji kutokana na kubakisha miezi sita katika mikataba yao.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Simba tayari imeanza kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji hao wanaomaliza mikataba yao kwa ajili ya kuwaongezea mipya itakayowabakisha.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kati ya wachezaji hao wapo waliokubali na kukataa, kati ya hao ni Chama ambaye inaelezwa amegoma kuongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo kwa kile kilichotajwa kutokuwa na furaha.

 

Aliongeza kuwa mwingine ni Kanda ambaye yeye anatajwa kurejeshwa TP Mazembe ya DR Congo iliyomtoa kwa mkopo wa mwaka mmoja wa kuichezea Simba unaomalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

“Simba hivi sasa ipo kwenye mipango ya mwisho ya kuwaongezea mikataba mipya wachezaji wake watatu ambao ni Mzamiru, Wawa na Shiboub baada ile ya awali kumalizika.

 

“Wawa na Shiboub walipewa mikataba ya mwaka mmoja ambayo inamalizika mwishoni mwa msimu, hivyo kutokana na viwango ambavyo wamevionyesha uongozi umeona ni vema wakawaongezea mkataba.

 

“Wawa hakuwepo kwenye mipango ya kuongezewa mkataba mwingine, lakini bidii yake ya kujituma na kutimiza wajibu wake ndiyo umesababisha aongeze mkataba huo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Katibu Mkuu wa Simba, Dkn Arnold Kashembe alizungumzia hilo na kusema: “Muda wa usajili bado na viongozi, wachezaji wote tumeelekeza akili zetu kwenye ubingwa wa ligi na baada ya hapo kila kitu kitajulikana.”

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave A Reply