The House of Favourite Newspapers

WATOTO FAMILIA MOJA WATEKWA

DAR ES SALAAM: Wakati wimbi la watoto kutekwa likiendelea kutikisa nchini huku Jeshi la Polisi likiendelea kuwatafuta, watoto Kulthum Ally (7) na Hidaya Ally (5), wakazi wa Geita, wamedaiwa kutekwa katika mazingira ya kutatanisha kwa siku tofauti, Amani linaripoti.  

 

Watoto hao walipishana siku nane kwa kupotea ambapo Hidaya alidaiwa kutekwa Septemba 24, mwaka huu mazingira ya nyumbani huku Kulthum akidaiwa kutekwa, Oktoba 3 mwaka huu alipokuwa akitoka shule.

 

Mtoto Kulthum alipotea akiwa katika mazingira ya shule, huku mtoto Hidaya akiwa ametoweka katika mazingira ya nyumbani kwao alipokuwa akicheza nje ya nyumba. Akisimulia kwa uchungu mama wa watoto hao, Lilian Ally alisema sintofahamu hiyo kwenye familia yake ilianzia kumkumba Septemba 24, mwaka huu baada ya Hidaya kutoweka nyumbani kwao saa 12 jioni.

 

“Nilimuacha dada wa kazi nyumbani mimi nikawa nimetoka kazini, niliporudi dada akaniambia alikuja mwanaume mmoja, akasema ni ndugu yangu akamrubuni na kutoweka naye,” alisema mama huyo na kuongeza “Dada aliniambia kwamba yeye alifikiri kuwa kweli ni ndugu maana alionesha kunifahamu mimi pamoja na baadhi ya ndugu zangu wengine.”

 

MWINGINE NAYE ATOWEKA

Alisema wakati wakiwa Oktoba 3, mwaka huu Kulthum alitoweka katika mazingira tata alipokuwa Shule ya FTM Islamic alipokuwa anarudishwa nyumbani kwa kutumia usafiri wa shule (school bus). Alisema siku ya tukio, tofauti na siku zote ambazo mwanaye anaenda na kurudishwa na gari hilo, alipata wasiwasi baada ya usiku kuingia bila ya Kulthum kuonekana.

 

AMTAFUTA DEREVA

Alisema alijaribu kuwasiliana na dereva wa school bus lakini cha kushangaza dereva huyo alisema kuwa siku hiyo mtoto huyo hakupanda gari lake.“Nilishtuka mno baada ya kuniambia kuwa Kulthum hakupanda gari lake na hajui alipo, akanishauri nijaribu kuwasiliana na walimu wanaweza kuwa na majibu mazuri kuhusiana na mwanangu,” alisema mzazi huyo. Alisema, aliendelea kumtafuta mtoto wake kwa kuwasiliana na walimu wa shule anayosoma mtoto wake ambapo hawakuwa na taarifa za kutoweka kwa mtoto huyo.

 

Alisema baada ya kupita saa 24 aliamua kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Magogoni mkoani humo na kupatiwa jalada la TAARIFA GE/ RB/5677/2018.

ASAURIWA KUMTAFUTA MZAZI MWENZAKE

Alisema, baadhi ya watu wake wa karibu walimshauri ajaribu kumtafuta baba wa watoto wake ambaye walitofautiana muda mrefu ambapo alipojaribu kufanya hivyo, hakuweza kupata ushirikiano kutoka kwa mzazi mwenzake. “Hakunipa ushirikiano wowote, nikawa naendelea tu kuwatafuta wanangu tangu Septemba 24 hadi leo. Naliomba Jeshi la Polisi linisaidie na Watanzania kwa ujumla ili niweze kuwapata wanangu popote walipo wakiwa hai,” alisema kwa masikitiko Lilian na kuongeza:

 

“Nimejaribu kusambaza mawasiliano yangu pamoja na vipeperushi vinavyoonyesha picha ya watoto wangu na kutumia mitandao ya kijamii kama Instagram, magrupu mbalimbali ya WhatsApp lakini hadi sasa bado sijapata fununu zozote walipo wanangu. Mwenye taarifa yoyote anitafute kwa namba 0658-542 263.”

 

Lilian alisema alibahatika kuzaa na baba wa watoto wake watoto hao wawili lakini mzazi mwenzake hakuishi naye kwa muda kutokana kushindwana tabia hivyo akabaki akilea watoto peke yake.

MAJIRANI WAPATA HOFU

Mmoja wa majirani wa mzazi huyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Doto alisema kitendo cha watoto hao kuchukuliwa na watu wasiojulikana kimewapa hofu mtaani hapo kutokana na kushindwa kujua wanaowateka watoto hao huwa wanakuwa na lengo gani. “Yani huwezi amini kwa sasa tuna hofu kweli hapa mtaani, hatujui wanaochukua watoto kama hivi wanakwenda kuwafanya nini, Mungu atusaidie sana. Tunaliomba Jeshi la Polisi litusaidie kuimarisha ulinzi na pia kuwasaka wale wote ambao wametekwa,” alisema jirani huyo.

 

MATUKIO YA UTEKAJI

Hivi karibuni yameripotiwa matukio mbalimbali ya watoto kutekwa ikiwemo lile la Idrissa Ally (13), mkazi wa Tegeta Masaiti jijini Dar, alitekwa alipokuwa akicheza na wenzake ambapo hadi sasa hajapatikana.

Kama hiyo haitoshi, mtoto Beuty Yohana (3) alitekwa lakini bahati nzuri alipatikana huko Kitunda nje kidogo ya jiji la Dar naye mtoto Gabriela Kilimba aliibwa akiwa amelala chumbani nyumbani kwao Ukonga Mazizini Dar na hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, hajapatikana.

 

MHARIRI

Ni vyema wazazi wakachukua tahadhari, wakawa makini na watoto wao hasa wanapokuwa wanacheza mitaani nje na nyumba zao pia polisi wazidishe ulinzi-Mhariri

Comments are closed.