The House of Favourite Newspapers
gunners X

Watoto Watoweka, Wakutwa Wamekufa

TUKIO la hivi karibuni lililoibua hofu kubwa ni la watoto wawili wa familia mbili wa Kijiji cha Nyamhela, Kata ya Mhongolo, Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, Hilda Deus (10) na Doroth Johanes (6) kutoweka kisha kukutwa wamefariki dunia, Risasi lina habari hii ya kusikitisha.

 

Watoto hao walitoweka nyumbani kwao masaa kadhaa Agosti 9 mwaka huu kisha baadaye walikutwa wakiwa wamefariki ndani ya bwawa la maji lililotokana na uchimbaji wa moramu.

 

Chanzo chetu cha kuaminika kililiambia Risasi kuwa, kitendo cha watoto hao kukutwa wakiwa wamefariki ndani ya bwawa hilo kiliibua mshituko kwa wakazi wa eneo hilo huku wazazi wa marehemu wakibaki na simanzi kubwa.

 

“Watoto hao walianza kutoweka, jitihada za kuwatafuta zikafanyika kwa masaa kadhaa na ndipo baadaye zikakutwa ndala zao pembeni mwa bwawa hilo na kubainika walikuwa ndani yake wakiwa wamekufa.

“Tunaomba serikali ione namna ya kulifukia bwawa hili kwa kuwa limekuwa ni hatari kwa maisha ya wakazi wa eneo hili,” alisema mtoa habari huyo aliyejitambulisha kwa jina la Hashim Juma.

 

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mhongolo, Emmanuel Nangale alisema tukio la vifo vya watoto hao limewasikitisha kwani si hasara kwa wazazi wao tu bali hata kwa taifa.

 

“Kwa kweli ni tukio la kusikitisha sana kwa watoto hao kukutwa wamefariki ndani ya dimbwi hilo, wito wangu kwa wazazi ni kuwa makini na malenzi ya watoto wao na kuhakikisha kila wanapokuwa wako salama,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:

“Kwa sasa bwawa hilo linatumika kwa shughuli za kilimo pamoja na kufyatua matofali. Hata hivyo kwa tukio hili hapaswi kunyooshewa kidole mtu yoyote kwa kuwa hiyo ni ajali kama ajali nyingine. “Kuhusu udhibiti wa mashimo hayo nimeshayatolea taarifa kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji.”

 

Akizungumzia tukio hilo, mmiliki wa bwawa hilo ambaye ni mzazi wa marehemu Hilda Deus, Deus Daud alisema tukio hilo limeacha simanzi katika familia yake huku akieleza kuwa, kwa madhara hayo yuko tayari sehemu ya bwawa lake hilo izibwe ili kuepusha hatari.

 

“Inauma sana, siku ya tukio baada ya mwanangu kutoka shule majira ya saa kumi, alipobadilisha sare zake alitoka na ndipo baadaye tulimkuta yeye na mwenzake wakiwa wamekufa kwenye bwawa hilo,” alisema mzazi huyo.

Naye baba wa Doroth, Johanes John, alimtupia lawama Deus kwa kuwapuuza wazazi wenzake waliompelekea barua ya kumtaka afukie shimo hilo.

 

“Sisi na mwenyekiti wa serikali ya mtaa tulishawahi kupeleka barua kwake ya kumtaka afukie shimo lake ili watoto wetu wasije kufa kwa kudumbukia, sasa hakufanya hivyo hadi leo mtoto wangu na wake umauti umewakuta, inasikitisha sana,” alisema John kwa uchungu.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, vifo vyao vimetokana na kudumbukia kwenye bwawa hilo la maji. Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huo na tunamuomba Mungu awape mioyo ya subira katika kipindi hiki kigumu.

Comments are closed.