The House of Favourite Newspapers
gunners X

Watoto Wawili Waacha Simanzi Kufa Siku 1

0

DAR: Watoto wawili waliofariki siku moja; Collins Kimaro (9) na Catherine Kimaro (4) kutokana na ajali ya moto Mei 3, mwaka huu, wameacha simanzi nzito wakati wakiagwa nyumbani kwao, maeneo ya Mabibo- Makuburi, jijini Dar.

 

Miili ya watoto hao iliibua simanzi hiyo kutoka kwa majirani na watu wa karibu wa familia ambao walihudhuria kwenye zoezi la kuaga kwa ajili ya kwenda kuzikwa nyumbani kwao Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Masikini jamani, angalia huyu mmoja alikuwa na miaka 9 tayari alikuwa kijana mkubwa tu na huyu mwingine alikuwa na miaka minne, daah inauma sana,” alisikika akilia mmoja wa waombolezaji huku waombolezaji wengine wakiwa kwenye sura za majonzi.

 

Akizungumza wakati wakiaga miili ya watoto hao juzi Alhamisi, baba yao mzazi, Christopher Kimaro alisema usiku alisikia kelele zikipigwa alipokuwa dukani kwake maeneo ya jirani na nyumbani kwake na alipokimbia haraka kurudi, alikuta nyumba yake ikiwa imeshika moto mkali.

 

“Siku ya tukio, mke wangu alikuwa amesafiri na msiba wa ndugu yetu huko Mpwapwa. Mimi huwa nafanya shughuli zangu jirani na hapa nyumbani kama kilometa kadhaa hivi, sasa nikiwa kazini kwangu muda wa saa nne hivi na nusu usiku, nikasikia kelele za moto, niliporudi ndipo nikakuta nyumba tunayoishi inaungua,” alisema.

 

Akizungumzia chanzo cha moto huo, mzazi huyo alisema anahisi huenda ulisababishwa na mshumaa.

“Kuna binti ambaye ni ndugu wa mke wangu huwa anabaki na watoto, sasa aliwasha mshumaa kwa sababu umeme ulikatika halafu akawa ametoka, sasa ule mshumaa uliwaka mpaka ukaisha na kushika kwenye nguo na kusababisha mlipuko mkubwa,” alisema mzazi huyo na kuongeza:

“Sasa nilipofika, watoto nilikuta wamelala na tayari moto kila sehemu ukiwa umetanda… majirani walikuja pamoja na kikosi cha zima moto lakini hatukufanikiwa kuwatoa watoto wala kitu chochote,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Makuburi, Moshi Hassani Kaftani alisema kuwa, tukio hilo limetokea katika moja ya nyumba zake ambayo imesababisha maafa kwa watoto hao wawili.

 

“Nilikuwa nimelala, nakumbuka ilikuwa usiku mwanangu akaja kuniamsha na kuniambia moto unawaka kwenye nyumba ya wapangaji.

“Nikatoka na kukuta moto mkubwa umeshika kila sehemu na majirani wakaja, nikawapigia simu polisi wa External wakaja na gari ya zima moto, walijaribu kuzima moto lakini ndio hivyo tena watoto wawili wamepoteza maisha na leo tunasafirisha kwenda Moshi kwa ajili ya mazishi,” alisema.

 

Baada ya zoezi la kuaga kukamilika, miili ya watoto hao ilisafirishwa kuelekea Moshi kwa ajili ya mazishi. Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi, Amina.

STORI: NEEMA ADRIAN, RISASI

Leave A Reply