Watu 14, wakiwemo watoto wawili, wamejeruhiwa nchini Msumbiji baada ya polisi kutumia risasi za moto na gesi ya kutoa machozi kutawanya mkusanyiko wa wafuasi wa upinzani waliokuwa wakimsindikiza kiongozi Venancio Mondlane jijini Maputo.
Mondlane, ambaye alipata asilimia 24 ya kura kwenye uchaguzi wa rais wa Oktoba mwaka jana, amekuwa akiitisha maandamano kupinga matokeo hayo, akidai yalikuwa ya wizi. Hata hivyo, maandamano hayo yamekuwa yakikabiliwa na nguvu za vyombo vya dola, hali iliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 320.