The House of Favourite Newspapers

ads

Watu 150 Wafariki Kwenye Mkanyagano Wakisherekea Sikukuu ya Halloween

0
Zaidi ya watu 150 wanaripotiwa kufa huko Korea Kusini katika mkanyagano uliotokea wakati wa Sherehe za Halloween mjini Seoul usiku wa kuamkia leo

Zaidi ya watu 150 wanaripotiwa kufa huko Korea Kusini katika mkanyagano uliotokea wakati wa Sherehe za Halloween mjini Seoul usiku wa kuamkia leo Jumapili Oktoba 30, 2022.

 

Vifo hivyo vimetokea wakati umati mkubwa wa vijana wakiwa wanasherehekea Sikukuu ya Halloween huko mjini Seoul ambapo walinaswa na kukandamizwa katika uchochoro mwembamba. Maafisa wanasema watu wengine 150 wamejeruhiwa katika mkasa huo mbaya kuwahi kutokea nchini Korea Kusini kwa miaka mingi.

 

Mkasa huo umetokea karibu na Hoteli ya Hamilton katika Wilaya ya Itaewon ambayo ni maarufu kwa burudani za usiku huku idadi kubwa ya watu wakiwa wamekusanyika katika uchochoro mwembamba karibu na hoteli hiyo.

 

Sherehe hizo za Halloween zilikuwa ndiyo za kwanza zinaanza kufanyika mjini Seoul ndani ya kipindi cha miaka mitatu baada ya serikali kuondoa vizuizi vya UVIKO-19.

 

Kwa mujibu wa mashuhuda, kuliibuka matukio ya ghasia muda mfupi kabla ya kutokea mkanyagano, huku Polisi waliokuwa wakifuatulia sherehe hizo za Halloween wakishindwa kudhibiti umati mkubwa. Kijana mmoja aitwaye Monn Ju-Young amelieleza Shirika la Habari la Reuters kuwa; “Kulikuwa na dalili zote kwamba kutakuwa na tatizo kwenye uchochoro kabla ya tukio.”

 

Wengine wameeleza jinsi walivyokuwa wakihaha kutoka katika umati uliokuwa umefurika, wakati watu wakirundikana juu ya wengine na wahudumu wa afya waliozidiwa na idadi ya waathirika wakiomba usaidizi kwa wapita njia.

 

Kwa mujibu wa maafisa wa zima moto, watu waliendelea kumiminika kwenye uchochoro mwembamba ambao tayari ulikuwa umefurika ukuta hadi ukuta, wakati wengine waliokuwa juu ya barabara yenye mteremko wakianguka na kuwaangusha wengine.

Leave A Reply