Watu sita akiwemo aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya klabu ya Simba, Muharami Sultan (40) wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za Kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilogramu 34.89.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma, Kambi Zubery Seif, Said Matwiko, Maulid Mzungu maarufu mbonde (54), John John maarufu Chipanda (40) na Sarah Joseph.
Akiwasomea hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi Grace Mwanga amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mery Mrio kuwa washtakiwa wote Kwa pamoja wanakabiliwa na mshtaka mawili ya kusafirisha dawa za Kulevya.
Amedai Oktoba 27,2022 eneo la Kivule jijini Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja walisafirisha dawa za Kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilogramu 27.10 .
Amedai katika shtaka la pili Novemba 4, 2022 maeneo ya Kamegele wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani washtakiwa hao kwa pamoja walisafirisha dawa za Kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilogramu 7.79.
Wakili amesema kuwa Upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo ameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Mrio amesema mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la dawa za kulevya na washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote na kesi imeahirishwa Hadi Desemba 5,2022