Watu Watatu Wafariki baada ya Lori kuacha Njia Kimara Stop Over Dar
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila amesema watu watatu wamethibitika kufariki dunia baada ya lori lililokuwa linatokea Kibaha kwenda Dar es salaam kuacha njia na kuparamia watembea kwa miguu, Madereva bajaji na bodaboda katika mataa ya Kimara Stop Over Jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo Februari 14, 2025 ambapo miili ya watu hao ilikandamizwa na lori.
Akiongea baada ya kufika eneo la tukio na kusimamia zoezi la kunyanyuliwa kwa lori na kontena lake ili kutoa miili, RC Chalamila ametoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivyo na amewashukuru wote waliotoa msaada wao kwenye ajali hiyo.
“Mpaka muda huu tumetoa miili mitatu ambayo inasemekana walikuwa Madereva pikipiki lakini pia tumetoa pikipiki ambazo kwa idadi ni nyingi kidogo kuliko Watu tuliowakuta na kwa mantiki hiyo taarifa ya Jeshi la Polisi itaweka bayana kuhusu idadi ya pikipiki, ajali imetokea saa ngapi, chanzo cha ajali na taarifa nyingine za msingi”