The House of Favourite Newspapers

Watu zaidi ya 70 Wapoteza Maisha na wengine kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kusababisha mlipuko

Watu zaidi ya 70 wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kupinduka na kusababisha mlipuko, tukio lililotokea Jumamosi, Januari 19, 2025, kaskazini mwa Nigeria. Shirika la Kitaifa la Dharura (NEMA) limethibitisha ajali hiyo iliyotokea katika jimbo la Niger.

Kwa mujibu wa taarifa za NEMA, watu 56 wamejeruhiwa, zaidi ya maduka 15 kuharibiwa, na juhudi za kukusanya miili ya waliofariki bado zinaendelea. Waathirika walioumia wamepelekwa hospitalini kwa matibabu.

Kumar Tsukwam, kamanda wa shirika la usalama barabarani katika jimbo hilo, alisema wengi wa waathirika walikuwa wakazi wenye kipato cha chini waliokimbilia kuchota mafuta yaliyomwagika baada ya lori kupinduka. Licha ya juhudi za mamlaka kuzuia umati, watu walivamia eneo hilo, hali iliyopelekea mlipuko mkubwa.

Ajali za mlipuko wa mafuta zimekuwa zikijirudia mara kwa mara nchini Nigeria, taifa linaloongoza kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika. Mwezi Oktoba 2024, mlipuko mwingine wa aina hiyo ulitokea katika jimbo la Jigawa na kusababisha vifo vya watu 147.

Hali ya maisha inazidi kuwa ngumu nchini humo, ambapo bei ya mafuta imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 400 tangu Rais Bola Tinubu alipoondoa ruzuku ya mafuta iliyodumu kwa miongo kadhaa, mara tu alipoingia madarakani Mei 2023.

Bologi Ibrahim, msemaji wa gavana wa jimbo la Niger, amewataka wakazi kujiepusha na tabia ya kuhatarisha maisha yao kwa kukimbilia malori ya mafuta yanayopata ajali.

ULINZI wa KUTISHA – UTAPENDA MSAFARA wa KIHISTORIA MWENYEKITI wa CCM TAIFA – RAIS SAMIA AKIINGIA…