The House of Favourite Newspapers

WATUHUMIWA 11 KIZIMBANI KISUTU KESI  YA UHUJUMU UCHUMI

Baadhi ya watuhumiwa  11 wakiwamo raia wawili wa Guinea waliopandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ya 
uhujumu uchumi kwa kukutwa na vipande 660 vya meno ya tembo.

 

 

WATU 11 wakiwamo raia wawili wa Guinea wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ya uhujumu uchumi kwa kukutwa na vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya shilingi bilioni 4.5.

 

Washtakiwa hao waliachiwa na kufunguliwa mashtaka mapya. Awali walikuwa wanakabiliwa na mashtaka hayo hayo ya uhujumu uchumi ambapo waliachiwa huru na Hakimu Mkazi, Maira Kasonde lakini baada ya kuachiwa walikamatwa ndani ya Masaa matatu tena wakapandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka mapya.

 

Wakiwasomewa mashtaka mapya mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizire, Wakili wa Serikali, Salim Msemo amewataja washtakiwa hao kuwa ni  Victor Mawalla, Calist Mawalla, Solomoni Kuhembe, Haruna Abdallah’ Kasa’, Abas Hassan ‘Jabu’,Ismail Kasa, Khalfan Kahengela, Musa Ligagabile, Kassim Said Ally Shariff na Fatoumata  Saumaolo raia wa Guinea.

 

 

Imedaiwa kuwa  washtakiwa kwa pamoja kati ya Aprili 6 na Juni 23, 2016 jijini Dar es Salaam, waliratibu na kusafirisha vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya USD 2,105, 181 ambazo sawa na bilioni 4.5 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria ya wanyama pori.

 

 

Imedaiwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao walijihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria ya wanyamapori ambapo wanadaiwa walisafirisha vipande hivyo.

 

Pia washtakiwa watano kati ya hao, Ally, Victor, Calist, Haruna na Abbas wanadaiwa kuwa walikutwa na vipande vya meno ya tembo kinyume na
sheria za wanyamapori.

 

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

 

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.

 

 

Hata hivyo washtakiwa hao walilalamika mahakamani hapo kuwa hiyo siyo kesi mpya ilifutwa Masaa matatu kabla hawajafunguliwa kesi hiyo mpya, hivyo waliomba kutendewa haki kwa sababu wanaumia gerezani na waliomba  kesi hiyo iende mahakama Kuu kwa  vile ni mda mrefu umeita wakiwa gerezani.

 

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 3, mwaka huu.

 

Comments are closed.