The House of Favourite Newspapers

Sita Kizimbani kwa Kukutwa na Pembe za Ndovu

WATU sita wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiwemo Hassan Likwena maarufu kwa jina la ‘Nyoni’, wakikabiliwa na mashtaka manne likiwamo la kukutwa na vipande 413 vya pembe za ndovu na viwili vya kiboko vyenye thamani ya Sh. bilioni 4.


Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla kutangaza kukamata vipande 413 vya pembe za ndovu na kukamatwa kwa Nyoni ambaye alimtaja kuwa alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu na serikali kutokana na kujihusisha na biashara haramu ya nyara za serikali.


Mbali ya Likwena (39) ambaye ni mkazi wa Kivule, wengine ni Bushiri Likwena mkazi wa Kitunda, Oliver Mchuwa (35), Salama Mshamu (21), mkazi wa Chamazi, Haidary Sharifu (44) a na Joyce Thomas (33).


Akiwasomea mashtaka,  Wakili Simon amedai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2017 kwenye maeneo tofauti mkoani Mtwara na Dar es Salaam kwa pamoja na kwa kushirikiana  walipokea  vipande 413 vya pembe za ndovu  vyenye thamani ya Dola milioni 1,755,000 za Marekani na vipande viwili vya meno ya kiboko vyenye thamani ya Dola 1,500 za Marekani.


Katika shitaka la pili, inadaiwa washitakiwa hao Septemba 3, mwaka huu maeneo ya Saku Chamanzi Wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na nyara za serikali ambavyo ni vipande 413 vya pembe za ndovu vyenye thamani ya Dola 1,755,000 za Marekani sawa na Sh. bilioni,  mali ya serikali pasipokuwa na kibali.


Pia inadaiwa katika shitaka la tatu, washitakiwa hao Septemba 3, mwaka huu maeneo ya Saku Chamanzi walikutwa vitu hivyo kinyume na sheria vyenye thamani ya Dola 1,500 za Marekani,  sawa na Sh. milioni 3.4.


Katika shitaka la nne la utakatishaji fedha, inadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari 2017 na Septemba 9, mwaka huu mkoani Mtwara na maeneo mengine ya Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walikutwa na vipande 413 vya pembe za ndovu vilivyo na thamani Sh. 1,755,000 na mbili za kiboko ambavyo kwa pamoja jumla yake ni zaidi ya Sh. bilioni nne, wakati wakijua ya kwamba upokeaji huo ni viashiria vya kosa tangulizi ambalo ni ujangili.

Comments are closed.