Mwili Wa Regina Aliyetoweka Ghafla Wakutwa Kwenye Shimo la Maji Taka, Ndugu Wadaiwa Kuhusika
Jeshi Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limesema kuwa limewakamata na kuwashikilia watuhumiwa wawili, Fred Rajabu Chaula na Bashir Richard Chaula kwa tuhuma za kula njama na kumuua Regina Rajabu Chaula miaka 62 mkazi wa Bahari Beach Kinondoni Dar es salaam na Denmark.
Mwanamke huyo anadaiwa alikuwa na kesi zake za madai Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi dhidi ya watuhumiwa na watu wengine na hivyo alipotea ghafla na hakuonekana tena tangu Desemba 13, 2024.
Jeshi la polisi lilifanya jitihada kubwa za kufuatilia na kuendelea kutilia mashaka maeneo na watu mbalimbali na ilipofika mnamo Januari 18, 2025 makachero wa Jeshi la Polisi walilazimika kubomoa shimo la maji machafu liliokuwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na kuukuta mwili wa marehemu Regina Rajabu
ukiwa umetupwa na kufichwa kwenye shimo hilo.
Kamanda Muliro amesema Uchunguzi wa kisayansi unaendelea juu ya tukio hilo baya na Jeshi la Polisi linalaani vikali vitendo hivyo na litahakikisha kila aliyeshiriki katika mauaji hayo ya kinyama anakamatwa na hatua kali za kisheria zinachukuliwa haraka dhidi ya watuhumiwa kwa kuwafikisha kwenye mamlaka zingine za kisheria.