Watuhumiwa Wizi wa Dhahabu Wafikishwa Mahakamani

WATUHUMIWA 10 wanaodaiwa kuwa ni wafanyabiashara wa madini wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya ambapo watano kati yao wamesomewa mashtaka tofauti ya uhujumu uchumi ikiwemo utoroshaji wa madini na wengine watano wamewekwa chini ya uangalizi wa mahakama kwa kipindi cha mwaka mmoja ili wawe na mwenendo mzuri.

 

Katika kesi ya kwanza ambayo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Andrew Scout, inawahusu watuhumiwa watatu ambao ni Mike Konga, Sauli Solomon na Emmanuel Kessy ambao wamesomewa mashtaka matatu.

Akiwasomea mastaka yao Wakili wa Serikali, Basilius Namkambe alisema shitaka la kwanza ambalo linawahusu watuhumiwa wote watatu ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

 

Alisema kuwa kati ya Juni Mosi na Juni 30, mwaka huu watuhumiwa hao walijipatia fedha za Zambia kiasi cha Kwacha 290,000 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa raia mmoja wa Zambia kwa kumuuzia dhahabu kinyume na Sheria.

Aidha, Wakili Namkambe alisema kosa la pili la watuhumiwa hao ni utakatishaji wa fedha kiasi cha kwacha 290,000 ambazo walizipata kwa udanganyifu kutoka kwa raia wa Zambia.

 

Watuhumiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na Wakili Namkambe akadai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa tena, ambapo Hakimu Andrew Scoult aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 23 mwaka huu itakapotajwa tena mahakamini hapo.

 

Katika kesi ya pili, mbele ya Hakimu Denis Luwongo, watuhumiwa wawili, Mike Konga na Sauli Solomoni wamesomewa mashtaka mawili ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha.

 

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Basilius Namkambe ameiambia Mahakama kuwa watuhumiwa kwa pamoja kati ya Juni Mosi na Juni 30 mwaka huu walijipatia fedha kiasi cha dola za Marekani 115,000 kwa njia ya udanganyifu baada ya kumuuzia Henry Clever, raia wa Ujerumani madini aina ya dhahabu kilo moja kinyume na sheria.

Watuhumiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa vile mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

 

Watuhumiwa wawili pekee ndio waliotimiza masharti ya dhamana na kuachiwa huru na watatu wamerejeshwa rumande hadi Ijumaa ya Septemba 13, kesi hiyo itakapotajwa tena na wao wametakiwa kufika na wadhamini.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa madini Stanslaus Nyongo ametoa wito kwa wafanyabiashara wa madini kuachana na biashara haramu za madini na badala yake wafanyebiashara hiyo kwa mujibu wa sheria ili kuepuka usumbufu ikiwemo kufilisiwa mali zao na kwenda jela. Mashataka hayo yalisomwa Septemba 9, 2019.


Loading...

Toa comment