The House of Favourite Newspapers

Wawa: Tulieni, AS Vita Watakufa Kwao

Pascal Wawa

BEKI wa kati wa Simba, Pascal Wawa raia wa Ivory Coast, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kusema kuwa watahakikisha wanacheza kufa na kupona katika mchezo dhidi ya AS Vita kwa lengo la kupata ushindi wa ugenini.

 

Simba ambayo ilitua DR Congo, jana Alhamisi tayari kwa mchezo wa pili hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita utakaopigwa Januari 18, mwaka huu imeondoka ikiwa na kikosi kamili isipokuwa Erasto Nyoni na nahodha John Bocco ambao ni majeruhi.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa muda mfupi kabla ya kuondoka, Wawa alisema hawawezi kuridhika na ushindi wa mchezo wao wa kwanza kwa kuwa bado wana safari ndefu kwenye michuano.

 

“Kwanza niwatoe hofu mashabiki wetu kwa sababu kazi ndiyo kwanza imeanza, hatupaswi kuridhika na matokeo ya mchezo uliopita, zaidi wanapaswa kuendelea kutuunga mkono ili tuweze kufanya vizuri kwenye mechi yetu ya ugenini.

 

“Tunawaheshimu wapinzani wetu kwa sababu ni timu kubwa na ina uzoefu wa kutosha lakini kwetu hakipaswi kuwa kigezo cha kuanza kuwahofia zaidi tunakwenda kwao kutafuta matokeo,” alisema Wawa.

 

Ikumbukwe wikiendi iliyopita, Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria na kufanikiwa kuongoza Kundi D, nyuma ya Al Ahly ya Misri ambao waliifunga AS Vita ya DR Congo.

Comments are closed.