Wawa: Waarabu hawatutishi

BEKI kisiki wa Simba, Pascal Wawa, amesema kuwa licha ya ratiba kuwa ngumu kwao, wanaamini watakwenda kishujaa kucheza na wapinzani wao JS Saoura ambao ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa.

 

Simba wanatarajiwa kuondoka kesho kuwafuata Waarabu hao wa Algeria wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 walipokutana nao kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa, mchezo wao wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Machi 9, Algeria.

 

“Kila siku tunatambua Kwamba tuna michezo mingi migumu kimataifa na ushindani ni mkubwa, kushindwa kupata matokeo kwenye mechi zetu zilizopita hesabu zetu ni kuona tunapata matokeo mechi zetu zilizo mbele yetu.

 

“Ushindi wetu utapatikana kwa kuwa kwa sasa tunaiheshimu kila timu ambayo tunakutana nayo, wachezaji wote tunacheza kwa ushirikiano hali inayotupa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mechi zetu zijazo hasa kwenye mashindano ya kimataifa ambayo yapo mbele yetu,” alisema Wawa.

 

Simba wapo Kundi D wakiwa Wanashika nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi sita, wapinzani wao JS Saoura wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi tano huku kinara akiwa ni Al Ahly mwenye pointi saba na anayeburuza mkia ni AS Vita akiwa na pointi nne.

Lunyamadzo Mlyuka,Dar es Salaam

Toa comment