The House of Favourite Newspapers

Wawanawake Wazuri Hawafai Kuolewa?

 UNA dhana ipo hususan kwa wanaume wengi kwamba, wanawake wengi wazuri hawafai kuolewa.

Wanaishibisha hoja yao kwa kutoa mifano, kwamba wanawake wengi walioolewa na kutulia kwenye ndoa zao ni wale wa daraja la kati. Wanawaita wa kawaida!

Wanaamini kuwa, wanawake wa aina hiyo wana mambo

mengi. Wana dharau, wanaotolewa macho na wengi, wana jeuri kwelikweli.

Katika uhalisia mwingine, wanaume wengi wamekuwa wakiwagwaya wanawake wazuri. Wengine wamekuwa wakiwatumia kama chombo cha starehe.

Utasikia mwanaume akiwaambia wenzake ‘kwa uzuri ule unafikiri yule ni mwanamke wa kuolewa?’

Haamini kwamba mwanamke mwenye figa ya kuwashtua wanaume, anaweza kutulia na kuolewa. Matokeo yake, wanawake hao, hujikuta wakikosa soko la ndoa.

Bahati mbaya sana, kuna baadhi yao wenyewe wamekuwa wakikubaliana na hali hiyo.

Wanaamua kuwa wanawake wa aina hiyo. Waburudishaji au wachangamsha genge kwa lugha rahisi. Wanatumika kulingana na mahitaji ya wanaume.

Leo atakuwa na huyu, kesho atakuwa na mwingine maana ana uhakika. Akiachwa leo, kesho ‘ashamteka’ mwingine. Ni bandika bandua.

Wanafanywa wa maonesho

Wanaume nao wanawatumia huku wakiwa na akili kichwani. Kwamba huyu ni mwanamke wa kutamba naye mtaani. Ni mwanamke wa maonesho.

Mwanamke wa kwenda naye ufukweni au sehemu za starehe. Kigezo kikubwa anachokitaka mwanaume ni kuwatambia wenzake kwamba ana ‘kifaa’.

Anamtumia pale anapokuwa na fedha. Zikikata anarudi kwa mwenzi wake wa siku zote. Yawezekana kabisa akawa na mkewe, anamtumia yule kama sehemu ya burudani. Yupo wake wa maisha.

Utakuta mkewe anamsifu kwamba ni wa kawaida. Hana makuu. Yeye amepata, amekosa, anamshukuru Mungu. Anamheshimu sababu anajua ndiye mstiri wake. Ndiye anayemfaa katika shida na raha.

Muhimu kujifunza

Mwanamke unapaswa kujitambua. Una kila sababu ya kujichagulia maisha ambayo yatakuwa na manufaa baadaye. Ukiamua kuwa chombo cha starehe, kweli utafanywa chombo cha starehe. Utavuna fedha nyingi kutoka kwa wanaume.

Watakubadilisha, watakupa kila unachotaka kutokana na umbo lako. Watakufurahisha lakini mwisho wa siku, umri nao utakutupa mkono.

Utakuja kushtuka umri umekuacha, unahitaji familia lakini humuoni wa kuzaa naye. Kila mwanaume ameshachukua hamsini zake na wewe mvuto huna tena.

Kuna maradhi. Yawezekana ukatumika na kujikuta umeingia kwenye matatizo makubwa ya afya.

Wakati huo hutamuona wa kukusaidia tena maana kila mmoja atakuwa anapambana na hali yake, kuilisha familia yake.

Ni aibu

Ni aibu mwanamke kufanywa chombo cha starehe. Kila mtu anakutumia halafu mwisho wa siku heshima yako itakuwa wapi? Wewe wanakutumia kisha wanarudi kwenye familia zao, familia yako wewe utaitengeneza lini?

Haohao wenye familia zao, wakishamaliza kukutumia, wataanza kukusema. Watakuona huna thamani. Watakufananisha na tambara la deki.

Umbo lisikuzuzue

Mwanamke mzuri anafaa kuolewa. Kikubwa ni kujitambua. Elewa kwamba, kuna maisha nje ya umbo na sura yako.

Kuna kutumika na kuachwa solemba. Jitambue. Jiheshimu na yatafakari maisha baada ya uzuri.

Wapo wazuri wengi tu wameolewa. Wametulia. Wanaheshimu ndoa na maisha yao ni mazuri. Jitathmini, acha kutumia muda wako vibaya. Unaweza ukawa mzuri na ukaolewa.

Maisha yana maana kama utatulia na uzuri wako, ukaijenga familia bora.

Ndoa ni heshima

Unapokuwa kwenye ndoa, mwanamke unaheshimika. Unakuwa na thamani mbele ya jamii inayokuzunguka na hata familia. Jitulize. Vaa mavazi ya staha.

Thamini utu kuliko mali. Thamani ya kuwa mwanamke itaongezeka kama utakuwa mrembo, mzuri lakini unayejiheshimu.

Kataa kufanywa mwanamke wa kiburudisho. Usikubali kutumika kwa namna yoyote.

Tubadilishane mawazo kupitia namba zilizopo hapo juu lakini pia waweza nicheki katika mitandao ya kijamii, Facebook na Instagram kwa jina la Erick Evarist. Twitter natumia ENangale.

Comments are closed.