The House of Favourite Newspapers

Wazanzibar Wote wakumbuke… Kubomoa ni Rahisi kuliko kujenga

0

Nimshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuishi leo, hatuna la kumpa isipokuwa kazi yetu iwe ni kumhimidi daima.

Leo nitazungumzia amani kwa wenzetu wa Wazanzibar ambao nawaambia kwamba mara zote kubomoa kitu ni rahisi kuliko kujenga na kama tusipokuwa makini kwa jinsi siasa zinavyofanyika V isiwani, ipo siku tutajuta na Zanzibar itaparaganyika, jambo tunaloomba Mungu aepushie mbali.

Nasema hivyo kwa sababu Zanzibar kuna makosa makubwa yamekuwa yakifanyika kila baada ya uchaguzi mkuu na kusababisha machafuko yanayochafua Tanzania nzima.
Ikumbukwe kwamba mwaka 2,001 kwa mara ya kwanza tulizalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni, Mombasa, Kenya, wengine Uingereza. Ilikuwa aibu kwa sisi tunaofikiri na kutafakari mambo.
Najiuliza; kwa nini kila uchaguzi mkuu kuna misukosuko ya kisiasa Zanzibar? Niliamini kwamba uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) mwaka 2010 ni suluhisho, lakini sasa sijajua mambo yatakuwaje siku zijazo.

Kugongana kwa viongozi wetu, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wake, Maalim Seif Sharif Hamadi kunaonesha kuna ufa mkubwa ndani ya visiwa hivyo.
Uraiani kuna jambo baya la raia kuvamiwa na watu wanaoitwa Mazombi. Hawa ni nani? Serikali iwapige vita kwani wanahatarisha amani ya nchi na kuonea raia wasio na hatia.
Kwa moyo wa dhati kabisa na nikizingatia utaifa, naomba mgogoro huu unaotikisa sasa Zanzibar baada ya kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu, ubabe uwekwe pembeni kwani unaweza kuturudisha kule tulikotoka ambako si kuzuri.
Lakini Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) iambiwe ukweli kwamba mambo ya kizembezembe siyo wakati wake wakati taifa linakimbia.

Uchaguzi wowote wanaousimamia lazima wawe makini kwa sababu kurudia uchaguzi mkuu ni gharama kubwa sana kwa taifa.
Hivyo, kizalendo kabisa, wanaopaswa kusimamia zoezi hilo wajitambue kuwa kosa lolote hasa kama ni la makusudi la kuvuruga uchaguzi, ni usaliti kwa walipa kodi.
Nishauri, kama wengine wanavyoshauri, suala hili linajadilika, pande zinazohusika zikae na kujadili kwa mapana huku utaifa ukipewa kipaumbele. Zec watazamwe kwa jicho kali kutokana na walichokifanya.

Vyama vyenye wafuasi wengi wakiongozwa na viongozi wao, Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM au Maalim Seif Sharif Hamadi wa CUF wajue wazi kwamba wasipoketi na kumaliza tatizo hilo, ‘jinamizi’ la historia ya ghasia kila baada ya uchaguzi, litainyemelea nchi, kitu ambacho ni kibaya na wengi hatupendi kitokee.
Kuna faida kubwa ya kuwa na serikali ya mseto (Coalition Government ) ya umoja wa kitaifa (National Unity) lakini la umuhimu ni kwamba itamjumuisha kila mmoja.
Nasema kweli kwamba migogoro ya kisiasa Zanzibar kumewafanya wananchi wa Visiwani kuwa na hisia tofauti kuhusu Muungano.
Sibishi kwamba kuna matatizo mengi ndani ya Muungano wetu, yatatuliwe. Hili lingefaa lijadiliwe kwa uwazi ili kuondoa dhana mbaya, mjadala uwe unaambatana na ukweli halisi usivutiwe na jazba ya kutaka ushindi.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply