WAZAZI KAENI CHONJO.. SIRI NZITO UTEKAJI WATOTO

WAKATI janga la watoto kuibwa na kutekwa katika mazingira ya kutatanisha likitikisa maeneo mbalimbali nchini huku wengi wakihoji kulikoni, binti aliyefahamika kwa jina la Teddy Stephano (26) Mkazi wa Matejoo mkoani Arusha amefichua siri iliyo nyuma ya matukio hayo. 

 

Teddy amefichua siri baada ya hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kumnasa akiwa ameiba mtoto wa kiume aliyekadiriwa kuwa na umri wa miezi 6 ambapo alipobanwa alisema, alifikia hatua hiyo baada ya kutafuta mtoto kwa muda mrefu bila mafanikio.

 

Akizungumzia tukio hilo ‘bichi’, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao alisema: “Aprili 6 mwaka huu majira ya saa 11 jioni Mtaa wa Igomelo Tarafa ya Kahama wakati askari polisi wakiwa doria walimkamata Teddy Stephano na baada ya kuhojiwa alikiri na kudai mtoto huyo amemuiba huko mkoani Arusha.

 

“Bado tunamshikilia kwa hatua zaidi pamoja na taarifa kwenda kwa polisi huko mkoani Arusha huku mtoto akiwa katika moja ya kituo cha kulelea watoto yatima Kahama ili kusubiria wazazi wake wapatikane,” alisema Kamanda Abwao.

 

KUNA MATUKIO MENGINE NYUMA

Tukio la Teddy kunaswa akiwa ameiba mtoto linaibua hofu tena ambapo katika siku za nyuma kidogo, wapo watoto ambao waliibwa na mpaka leo haijulikani walipo, jambo linaloibua swali la kwamba, watoto hao wanapelekwa wapi?

 

Baadhi ya watoto ambao walikumbwa na balaa hili ni pamoja na Beauty Yohana (3) wa Kimara jijini Dar ambaye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha kabla ya baadaye kupatikana huku kukiwa na madai kuwa ilikuwa apelekwe kwenye mambo ya kishirikina.

 

Mwingine aliyetekwa kimafia na mpaka leo hajulikani alipo ni mtoto Idrissa Ally wa Tegeta-Masaiti jijini Dar ambaye alichukuliwa na watu wasiojulikana kisha kupakizwa kwenye gari aina ya Toyota IST na kutokomea naye.

 

Wakati wazazi wa Idrissa wakilia wasijue aliko mtoto wao mpendwa, mtoto mwingine aitwaye Gabriela Kilimba (3) aliibwa akiwa amelala chumbani, nyumbani kwao Ukonga-Mazizini jijini Dar. Naye baadaye alipatikana katika mazingira ya kutatanisha.

CHANZO CHA MATUKIO HAYA

Kufuatia matukio hayo, kama alivyoeleza Teddy (binti aliyekamatwa na mtoto Shinyanga), inaonekana baadhi wanafikia hatua ya kuiba watoto kutokana na shauku ya kuitwa mama huku wakiwa hawana uwezo wa kunasa mimba.

 

Sheila Juma ambaye ni Mkazi wa Sinza jijini Dar anasema kuwa wimbi hili la kupotea kwa watoto hasa wadogo linachangiwa na wanawake ambao wametafuta watoto kwa udi na uvumba lakini wamekosa.

 

“Haya matukio ya wamama kukamatwa kwa wizi wa watoto yamekuwa yakiibuka kila mara na nadhani hawa ndiyo wanafanya tatizo hili kuwa kubwa. Kama umetafuta mtoto na umekosa kwa nini usikubaliane na hali hiyo mpaka ufikie hatua ya kuiba watoto wa wenzako?” alihoji mama huyo.

 

MAMBO YA KISHIRIKINA

Aidha imebainika kuwa, mbali na kuwepo kwa wanawake ambao wanaiba watoto ili kupata ile sifa ya kuitwa mama, wapo ambao hufanya hivyo ili kuwatumia kwenye masuala ya kishirikina. Hilo linashibishwa na tukio la mtoto Beauty Yohana (3) aliyeibwa kisha kupatikana akiwa na binti aliyefahamika kwa jina la Angel Vincent (19) aliyedai alidhamiria kumpeleka kwa bibi yake anayefanya mambo ya kishirikina.

 

“Kuna uwezekano mkubwa watu wenye imani za kishirikina wanahusika na utekaji wa watoto, wazazi wanatakiwa kuwa makini sana kwani dunia sasa inaelekea kubaya. Kama mtu anaweza kumchukua mtoto wa mwenzake na kwenda kumfanyia makafara, hiyo ni hatari sana kwa ustawi wa jamii,” alisema Sabuni Kasua wa Kimara jijini Dar na kuongeza: “Nchi yetu ni yenye amani na utulivu, watu wasituletee mambo ya ajabu ambayo hatujayazoea.”

 

KUNDI LA MAFIA

Wengine wanaotajwa kuhusika na matukio ya utekaji na wizi wa watoto ni ‘mafia’ ambao wamekuwa na tabia ya kuchukua watoto ‘kimafia’ kisha baadaye wanapiga simu kwa wazazi wao kutaka wapewe pesa ili wawarejeshe.

 

POLISI ATOA TAHADHARI

Kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi mara kadhaa limekuwa likitoa tahadhari kwa wazazi kuwa makini na watoto wao kila wanapokuwa ili kuwaweka mbali na makundi ya watu ambao wanatajwa kuhusika kwenye utekaji na wizi wa watoto. Aidha Kamanda Abwao (RPC Shinyanga) ametoa wito kwa watu wenye matatizo ya kiafya yanayowafanya wakose watoto kufuata njia sahihi za kukabiliana na hali hiyo kuliko kuiba watoto wa wenzao.

Stori: Paul Kayanda, RISASI MCHANGANYIKO


Loading...

Toa comment