The House of Favourite Newspapers

Wazee wa ‘Nitumie kwa Namba Hii’ Wanaswa Dodoma

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanikiwa kuwakamata watu kumi wanaojihusisha  na usajili laini za simu kwa kutumia vitambulisho vya watu wengine na kuzalisha laini nyingi kwa kitambulisho kimoja bila ridhaa ya mwenye kitambulisho.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, amesema kuwa laini hizo  wamekuwa wakiziuza kwa wahalifu  na watu wasio na vitambulisho ambao ni wahalifu.

Aidha, Muroto ameongeza kuwa wamewakamata wahamiaji  haramu wanne ambao ni raia wa Ethiopia na kwamba raia hao wanne walikamatwa katika eneo la Chipolo wilayani Mpwapwa wakiwa wanasafirishwa katika basi Namba T.112 ATC, SCANIA, Bus la Kampuni ya Premiere  Line linalofanya safari  kutoka Mwanza kwenda Mbeya.

Muroto ameongeza kwamba kwa  kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa yote wameanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo sasa wanalisaidia jeshi la polisi kuwaibua wahalifu wote katika mitaa yao na wapokeaji wa mali zinazotokana na uhalifu.

Aidha, amewataka madereva kuheshimu sheria za usalama  barabarani na kwamba anayetembea kwa miguu ana haki ya kisheria kama dereva anaye endesha barabarani.

Naye, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Kitengo  cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma Methew Benjamin,  amesema wameamua kujikita katika utoaji wa elimu zaidi  ya usalama barabarani hasa katika vivuko vya waenda kwa miguu ambapo zaidi ya asilimia 76 ya ajali za barabarani hapa nchini husababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na uzembe  wa madereva.

Pia katika mahojiano mbalimbali, watembea kwa miguu wamesema kuwa  hawana elimu ya kutosha juu ya vivuko vya watembea kwa miguu huku wengine wakitoa ushauri kwa madereva kufuata sheria za barabarani.
Na: Faustine Gimu Galafoni, Dodoma. 

Comments are closed.