The House of Favourite Newspapers

WAZIMBABWE WASUBIRI KIONGOZI MWINGINE BAADA YA MUGABE

0
Zimbabwe
Wananchi wa Zimbabwe wakisherehekea katika mitaa ya Harare kung’oka kwa Mugabe.

WANANCHI wa Zimbabwe hivi sasa wana shauku ya kumjua kiongozi wao mpya baada ya Robert Mugabe kuachia ngazi ya urais wa nchi hiyo kufuatia kuitawala kwa miaka 37.

 

Enzi za Mugabe zilikoma jana katika tangazo lililotolewa  katika kikao cha pamoja cha bunge ambalo lilikutana ili kumfungulia mashtaka rais huyo mwenye umri wa miaka 93.

 

Mitaani,  watu walishangilia kukoma kwa utawala wake waliouita wa kikatili.  Magari yalipiga honi na ving’ora kwa furaha, kushangilia mwisho wa utawala huo.

 

Rais anayetegemewa kuchukua nafasi ya Mugabe ni Emmerson Mnangagwa, ambaye alifukuzwa mwanzoni mwa mwesi huu katika nafasi yake ya makamu wa rais, jambo ambalo liliwaudhi wakuu wa jeshi na hivyo kuingilia na kumng’oa Mugabe.

 

Mnangagwa aliwahi kuwa ‘mshikaji’ mkuu wa Mugabe, lakini pia alikuwa mpinzani mkuu wa mke wa Mugabe, Grace, katika mbio za kutaka kumrithi Mugabe.

 

“Mimi, Robert Gabriel Mugabe… natoa barua yangu ya kujiuzulu… mara moja,” alisema katika barua iliyosomwa na Spika wa Bunge, Jacob Mudenda.

 

“Uamuzi wangu ni kujiuzulu kwa utashi wangu,” alisema, “kwa kutia maanani maslahi ya watu wa Zimbabwe na nia yangu ya kuhakikisha mabadiliko ya madaraka yanafanyika kwa amani na utulivu.”

 

Watu walionekana wamefurahi mitaani wakichana na kuondoa picha za Mugabe sehemu mbalimbali na wakishutumu utawala wake waliosema ulikuwa wa kikatili.

 

Chama tawala cha Zanu-PF  kilisema Mnangagwa aliyeondoka Zimbabwe baada ya kufukuzwa na Mugabe, atatajwa kuwa rais wa muda.

 

“Mnangagwa… atarudi katika nafasi yake mnamo saa 24 zijazo na ataapishwa kuwa rais wa muda kwa siku 90,”alisema msemaji wa chama hicho, Simon Khaya Moyo, jana.

 

Kujiuzulu kwa Mugabe kulikamilisha wiki nzima iliyoshuhudia jeshi likikamata uongozi wa nchi na makumi ya maelfu ya Wazimbabwe wa kawaida wakiandamana mitaani kuonyesha kumchukia Mugabe.

 

 

Leave A Reply