WAZIRI AIBUA KIKOMBE CHA BABU WA LOLIONDO

WAZIRI wa Nishati Dk. Medard Kalemani, mwishoni mwa wiki iliyopita aliibua upya ishu ya kikombe cha Babu wa Loliondo baada kufika katika Kijiji cha Samungena Digodigo Wilaya ya Ngorongoro na kuwasha umeme kwa mara ya kwanza, zoezi lililofanyika nyumbani kwa Mzee Ambilikile Masapila ‘Babu wa Liliondo’. 

 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na viongozi wengine pamoja na wananchi.

 

Akizungumza nyumbani hapo Jumamosi iliyopita wakati wa kuzindua Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu, Dk. Kalemani alisema amewasha umeme kwa mara ya kwanza nyumbani kwa babu wa kikombe kama ishara ya kufungua maendeleo mapya wilayani humo na hakufika pale kupata kikombe.

 

Aidha, aliwaagiza makandarasi wa kampuni ya Nipo Group wahakikishe ndani ya mwezi mmoja wamesambaza umeme huo Kata ya Samunge na Digodigo ili wananchi waitumie fursa hiyo kujipatia maendeleo.

Alisema serikali imetoa zaidi ya Sh. bilioni 40 kwa ajili ya umeme, hivyo ni vema kila mwananchi ahakikishe anawasha nyumbani kwake umeme kabla ya kulazimishwa. Pia aliagiza makandarasi hao kuajiri vibarua wasiopungua 60 ili kazi iende kwa haraka.

 

Naye Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Willium Ole Nasha, alishukuru Serikali kupeleka umeme Ngorongoro na kuuzindua rasmi. Kwa upande wake Ambilikile Mwasapila (Babu wa Kikombe) aliishukuru Serikali kumwashia umeme nyumbani kwake kwani ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu.

 

Alisema hatua hiyo ni ishara ya kutimia kwa ndoto yake anayoonyeshwa na Mungu kila mara kuwa Tanzania ni kioo cha Afrika.

“Sasa hizi ndizo ishara, zimeanza kuonekana,” alisema babu huyo. Babu wa Kikombe alikuwa maarufu miaka ya nyuma kwa kutoa kikombe cha dawa aliyodai inatibu kila ugonjwa ambapo maelfu ya watu wakiwemo mawaziri walimiminika kunywa dawa hiyo aliyodai alioteshwa na Mungu.

 

Hata hivyo baada ya zoezi hilo, wananchi wengi mtaani na kwenye mitandao ya kijamii walianza kujadili upya kikombe cha babu huku wengi wakihoji kiliishia wapi. “Daah! Ila huyu mzee alipata hela kupitia kile kikombe chake, naona sasa hivi mambo yake supa, shavu dodo na umeme emepelekewe,” alisema Shabani wa Sinza jijini Dar baada ya kuona picha ya mzee huyo akiwa amenona.


Loading...

Toa comment