The House of Favourite Newspapers

Waziri Ajiuzulu kwa Kusafiri Kifahari Kuhudhuria Kutawazwa kwa Mfalme Charles III

0
Waziri wa mambo ya nje wa Papua New Guinea, Justin Tkatchenko.

WAZIRI wa mambo ya nje wa Papua New Guinea, Justin Tkatchenko amejiuzulu baada ya kashfa ya matumizi ya fedha ya ujumbe rasmi wa nchi hiyo uliohudhuria kutawazwa kwa Mfalme Charles III.

Justin Tkatchenko alisafiri na binti yake Savannah, ambaye alichapisha kwenye mtandao wa TikTok kuonyesha safari yake kwenye ndege ya daraja la kwanza pamoja na kuonekana akifanya manunuzi mengi nchini Singapore.

Siku ya Jumatano, aliwataja wakosoaji wake kuwa “wanyama waliopitwa na wakati”. Maoni ya Bw Tkatchenko yalizua maandamano katika mji mkuu wa Port Morseby siku ya Ijumaa nje ya Ikulu ya Bunge.

Papua New Guinea ni taifa la Jumuiya ya Madola huko Pasifiki ambalo Mfalme Charles ni mkuu wake wa serikali.

Tkatchenko alisema katika taarifa Ijumaa kwamba “amejiweka kando” baada ya kushauriana na Waziri Mkuu James Marape.

Aliongeza kuwa anataka kuhakikisha matukio ya hivi majuzi hayaingiliani na ziara rasmi za Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

Tkatchenko na bintiye walikosolewa kwa kusafiri na maafisa wasiopungua 10 kushuhudia kutawazwa kwa Mfalme Charles, kwa gharama ya karibu dola 900,000, kwa mujibu wa gazeti la Post-Courier.

Msemaji wa serikali Bill Toraso alilithibitishia shirika la habari la Reuters kuwa wafanyakazi wake 10 walikuwa wamesafiri kwenda London, pamoja na wageni 10. Katika video hiyo ambayo imefutwa, Savannah alirekodi ziara yake katika maduka ya kifahari ya Singapore na mlo wake katika mgahawa wa daraja la kwanza alipokuwa njiani kuelekea London.

Leave A Reply