Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-10

ILIPOISHIA IJUMAA:
“Mzee Mgorosi akaguna. Alionesha waziwazi kufadhaika. Kwa shingo upande akaniambia: “Sawa bwana mdogo, nitawaambia wenzangu maneno yako.”
Nilikuwa sina mpango wa kuondoka alfajiri. Ningeondoka mchana.
SASA ENDELEA…

Lakini ile shughuli ya kichawi niliona haikuwa na maana, ndiyo nikatoa hoja ya kuondoka. Wakati ule nina huzuni ya kifo cha babu yangu, nikacheze ngoma ya nini?
Kama walikasirika na wakasirike, nikajiambia.

Kwa kutaka kuwakwepa wazee hao wasije wakaniharibia safari yangu, niliondoka usiku nikaenda kulala hotelini Nzega. Asubuhi yake nikaondoka kurudi Dar.

Siku iliyofuata nikaenda kazini. Ule mfuko alionipa babu niliondoka nao. Na mimi niliuweka uvunguni mwa kitanda bila mke wangu kujua. Siku mojamoja nilikuwa nikiutoa kwa siri kuufuta vumbi.

Ulikuwa ni wakati wa kukaribia uchaguzi mkuu. Mke wangu akanishauri nigombee nafasi ya kuteuliwa kugombea ubunge wa jimbo la kwetu Nzega.

Wazo lake lilikuwa zuri na nililiunga mkono. Nilikuwa mwanachama wa chama tawala na kadi yangu nilikuwa ninayo. Niliikatia Chuo Kikuu cha Mlimani.

Wakati ule nikiwa chuo kikuu nilijishughulisha sana na siasa hasa baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi. Tulikuwa na tawi letu la chama tawala ambapo tulikuwa tunaweka vikao vyetu na kujadili mambo ya siasa.

Baada ya kumaliza masomo, nilikumbana na changamoto za maisha nikayaacha mambo ya siasa. Baada ya mke wangu kunishauri nigombee ubunge ndipo nilipoikumbuka kadi yangu. Niliitafuta, nilipoiona nilikwenda kuilipia kwa vile nilikaa nayo kwa muda mrefu bila kuilipia ada.

Baadaye nilikwenda kumueleza dhamira yangu mkuu wangu wa kazi.
“Ni uamuzi mzuri,” akaniambia na kuniuliza.
“Unataka ugombee jimbo gani?”
“Jimbo la kwetu Nzega.”

“Watu wa Nzega wanakufahamu vya kutosha?”
Swali lake lilinizindua kidogo kwa sababu sikuwahi kufikiria juu ya kufahamika kwangu kwa watu wa Nzega.

Kama nilikuwa ninafahamika ilikuwa ni kidogo. Sehemu kubwa ya maisha yangu ilikuwa ni kijijini kwetu Mbogwe. Kwa vile nilikuwa ninahitaji kura za Wananzega wote, niliona nitakuwa na kazi kubwa ya kujinadi kwa wapigakura wangu ili wanifahamu na kunikubali.

Mkuu wangu wa kazi alinipa moyo na kunitaka nijaribu bahati yangu.
Siku chahe baadaye niliomba ruhusa ya siku kadhaa kazini kwangu nikaenda Nzega kujitambulisha kwenye ofisi za chama chetu na kutangaza nia.

Baadaye nilifahamishwa kuwa kulikuwa na watangaza nia wenzangu zaidi ya kumi ambao walitarajiwa kupita katika mchakato wa kura ya maoni ya wanachama wa chama chetu ili kumpata mgombea atakayekubalika.

Nilikuwa na tamaa ndogo sana ya kupita katika mchakato huo kwa sababu ya uchanga wangu katika siasa na kutofahamika sana kwa watu wa Nzega. Lakini sikuvunjika moyo.
Nilikwenda kijijini kwetu Mbogwe nikakutana na mzee Mgorozi nikamueleza dhamira yangu.

“Lakini bado ni mwenzetu?” Mzee Mgorozi akaniuliza akiwa amenitolea macho.
“Mimi bado ni mwenzenu na ahadi yangu bado ipo palepale.”
“Kwani mke wako yuko wapi?”
“Yuko Dar. Yeye hawezi kuja huku mara kwa mara kwa sababu yuko kazini.”
“Lakini tayari ni mjamzito?”

“Bado. Mwaka wa mwisho ni huu tu. Siku hizi tunakwenda kizungu. Unapanga ni wakati gani mnataka mzae.”

“Sasa wewe ukiwa mbunge utaweza kushirikiana na sisi?”
“Bila shaka yoyote. Nitaendelea kuwa nanyi kama babu yangu alivyoniusia.”
“Sasa leo utakuja uwanjani usiku?”
“Nitakuja.”

Mzee Mgorozi akafurahi nilipomwambia nitafika kiwanjani.
Yale maneno yangu alikwenda kuwaeleza wenzake. Wakanisubiri makaburini saa nane usiku. Waliponiona nimefika hawakuamini. Nilikuwa nimevaa kaniki yangu huku mkoba wa uchawi niliokabidhiwa na babu ukiwa kwapani.

“Karibu mjukuu,” Bi Shali akanikaribisha kwa furaha.
Ile kaniki niliyovaa pamoja ule mkoba wa uchawi niliouweka kwapani, uliwafanya waone nilikuwa bado ni mwenzao.

Loading...

Toa comment