The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-12

0

ILIPOISHIA IJUMAA:

Tulikuwa tunakwenda kwenye kila kata ambako wanachama walikuwa wanatusubiri.

Kila mgombea alikuwa anasimama na kuwaeleza wananchama kwa nini anataka ateuliwe yeye na asiwe mwingine?

Unapojieleza inabidi utoe maelezo yanayoonesha kuwa wewe ni zaidi ya wenzako kielimu, kiuwezo na kiuzoevu.

SASA ENDELEA…

Siku ile niliamini kuwa uchawi wa akina mzee Mgorozi ulifanya kazi kwani wagombea wenzangu walibabaika sana kujieleza. Ni mimi peke yangu niliyeweza kujieleza vizuri na kupigiwa makofi. Jicho la kila mwanachama lilikuwa likinitazama mimi kwa haiba.

Nikayakubali maneno ya mke wangu kuwa nilikuwa na mvuto na haiba ya kuwa mbunge, vinginevyo wale watu wasingenitazama namna ile.

Katika kata zote tulizokwenda ni mimi peke yangu niliyeonekana kung’ara. Wenzangu hawakutazamwa mara mbili. Ilikuwa kama vile kile kinyesi tulichokiacha siku ile mbele ya ofisi za chama chetu, kilikuwa kimewatapakaa miilini mwao.

Baada ya zoezi kukamilika, nikatangazwa kuwa mshindi wa kura ya maoni hivyo kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Nzega.

Katika kipindi hicho, nilikuwa nimeomba likizo kazini kwangu nikahamia Nzega pamoja na mke wangu. Nilitafuta nyumba ya kupangisha katikati ya mji huo.

Kule kijijini kwetu nilikuwa ninakwenda siku mojamoja. Lakini hata siku moja sikuwahi kwenda na mke wangu. Wala sikuwahi kuwajulisha wale wazee wachawi kwamba mke wangu nilikuwa naye.

Madhumuni yangu ya kupangisha nyumba na kuweka makazi yangu ni kutaka watu wa Nzega wanijue, wanizoee na waone ni mwenzao.

Hata hivyo, licha ya kushinda katika kura ya maoni, bado nilikuwa na wasiwasi kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi wenyewe kwani kulikuwa na wagombea ubunge watatu wa vyama pinzani ambao walikuwa maarufu.

Hao walikuwa wakinipa wasiwasi hasa vile ambavyo walikuwa wanakubalika sana kwa wananchi wa Nzega. Mmoja wa wagombea hao alitoka katika chama chetu baada ya mimi kumshinda katika kura ya maoni. Akaona kulikuwa na mizengwe hivyo akaamua kuhama chama.

Kikaanza kipindi cha kampeni. Kwa sababu nilikuwa nimeshajiingiza kwenye siasa, nikaamua kuacha kazi ili nipate nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo za siasa.

Lakini mke wangu alikuwa akiendelea na kazi na alikuwa akija Nzega mara mojamoja.

Kipindi cha kampeni kilikuwa kigumu. Kuna siku nilikuwa nafanya mikutano miwili kwa siku. Mikutano yangu ilikuwa haijazi watu sana kama mikutano ya vyama pinzani. Hilo nalo likanipa wasiwasi.

Siku moja jioni baada ya kumaliza mikutano, nikaenda kijijini kwetu kuwaona wale wazee wachawi, wakaniambia nilitakiwa kwenda kuziwangia pembe nne za Mji wa Nzega wakati wa usiku ili kuwapata vizuri watu wa mji huo.

Wachawi hao wakanisaidia. Usiku huo tuliuzunguka Mji wa Nzega. Tuliweka uchawi wetu katika pembe nne za mji huo. Siku iliyofuata nikaona watu wakijazana kwenye mikutano yangu.

Sasa badala ya kufanya mikutano kwenye mitaa kama ambavyo nilikuwa nafanya, nikawa nafanya mikutano kwenye viwanja vikubwa vya mji na watu walikuwa wanajaa utadhani ni mikutano ya kampeni ya urais.

Jambo hilo likanipa moyo. Mara kwa mara nilikuwa ninakwenda kule kijijini na kuwapa pesa za matumizi wale wazee ili wazidi kuniwangia nipate ushindi.

Siku ya uchaguzi ilipowadia wasiwasi ulinianza upya. Nilikuwa nikijiambia katika uchaguzi huo kulikuwa na kushinda na kushindwa.

Kama nitashinda lilikuwa ndiyo lengo na madhumini. Lakini kama nitashindwa si tu ningepata fedheha pia ningepata hasara kubwa kutokana na pesa nyingi nilizozitumia katika  kampeni.

Bado maisha yangekuwa magumu kwani nilikuwa nimeshaacha kazi kwa kutarajia kuwa ningeshinda ubunge. Yale matumaini yangu kuwa ningeshinda ubunge yalikuwa yamefifia ghafla.

Zoezi la upigaji kura liliendelea hadi muda uliokuwa umepangwa kumalizika. Nilikuwa nikizunguka katika vituo mbalimbali vya upigaji kura kuona kama kulikuwa na dosari zozote zilizojitokeza.

Siku ile nilikunywa chai saa tano, tena kwa kuhimizwa na mke wangu aliyekuwa Dar ambaye nilikuwa nikiwasiliana naye wakati wote. Kama si yeye kunihimiza, nilishausahau utaratibu wa kunywa chai asubuhi kutokana na kihoro nilichokuwa nacho.

Leave A Reply