Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-13
ILIPOISHIA IJUMAA:
Jambo ambalo sikulitarajia ni taarifa niliyoipata nikiwa bungeni kuwa rais alinitangaza kuwa mmoja wa mawaziri wake katika baraza lake la mawaziri aliloliunda mara tu baada ya kuapishwa kuwa rais.
Nikawa kwenye sherehe nyingine ya kuteuliwa kuwa waziri. Sikuwa peke yangu, karibu wote tulioteuliwa uwaziri tulikuwa tupo bungeni.
SASA ENDELEA…
Sasa heshima yangu haikuwa ya ubunge pekee, ilikuwa ya ubunge na uwaziri. Sitapenda kutaja nilikuwa waziri wa wizara gani lakini ilikuwa wizara nyeti. Sikuweza kujua rais alifikiri nini mpaka akaamua kuniteua mimi kushika wizara ile.
Asubuhi ya siku iliyofuata nikawa Dar kwenye viwanja vya ikulu, mimi na mawaziri wenzangu kwa ajili ya kuapishwa.Sote tulikula kiapo cha utii kwa rais, kulinda katiba, kutekeleza majukumu yetu kwa uaminifu na kutotoa siri za serikali nje.
Kilichofuatia baada ya hapo ni kukabidhiwa wizara zetu. Kila waziri alipewa gari lake ambalo angelitumia katika majukumu yake ya kila siku pamoja na nyumba ya kuishi.
Ndipo nilipoanza kazi yangu ya uwaziri. Siku ya kwanza nilipoingia ofisini mwangu nilikutana na wafanyakazi wa wizara yangu, tukatambuana na wakanipongeza kutokana na kuteuliwa kwangu kushika wadhifa huo. Siku ile ilikuwa ni ya furaha kwa wafanyakazi wote.
Jioni niliporudi nyumbani, mke wangu naye alikuwa akinisubiri kunipongeza. Alikuwa ametayarisha vinywaji, tukakaa sebuleni na kuanza kunywa na kuzungumza.
“Nakushukuru mke wangu kwa kunipa wazo ambalo leo limeniwezesha kuwa waziri,” nikamwambia mke wangu.
Uso wa mke wangu ulitabasamu kwa dhati.
“Lakini wewe ulianza kukata tamaa,” akaniambia.
“Kila nilipoonesha kukata tamaa, wewe ulinipa moyo nikazidi kusonga mbele.”
Tukacheka.
“Baada ya kushinda ubunge, rais amekupa na uwaziri, kwa kweli una bahati sana mume wangu,” mke wangu aliendelea kunipongeza.
“Lakini majukumu ya uwaziri ni makubwa, natakiwa kuwa makini sana.”
“Ninajua kuwa utakuwa makini. Lakini umeonaje leo ulipokalia kiti chako?”
“Oh nilifurahi sana.”
“Sasa zingatia sana bidii ya kazi mume wangu. Ulitaka Mungu akupe nini tena!”
“Bidii ni muhimu ili nioneshe mfano katika wizara yangu. Nitafanya kazi mchana na usiku iwapo ni lazima.”
Tukacheka tena.
Ofisi ya uwaziri ilikuwa tamu lakini pia ilikuwa chungu. Siku za mwanzomwanzo nilijikuta nikikabiliwa na changamoto nyingi za kazi. Lakini taratibu nilionekana kuizoea kazi yangu na kukabiliana vyema na majukumu yangu ya kila sku.
Katika kipindi cha bajeti ambacho huwapa taharuki mawaziri, nilianza kupata wasiwasi, japokuwa bajeti ya wizara yangu ilikuwa ikiandaliwa na wataalam wa wizara yangu wakiwemo wanasheria na wataalam wa uchumi.
Mawaziri ambao walitangulia kuwasilisha bajeti za wizara zao bungeni, niliona jinsi walivyokuwa wakihenyeshwa na wabunge. Bajeti ya wizara moja ilikwamishwa kabisa.
Hali ile ilinitia hofu na wasiwasi. Nilichokuwa nataka mimi ni kupitishwa kwa wizara yangu bila longolongo na si kupitishwa tu bali nilitaka pia nipongezwe na wabunge.
Hapo ndipo nilipoukumbuka mkoba wangu wa uchawi ambao nilikuwa nimeuweka uvunguni mwa kitanda changu.
Ilipofika usiku, niliutoa uvunguni. Nilivizia mke wangu akiwa usingizini ndipo nilipoamka na kuutoa. Nilitoka nao uani na kutoa vilivyokuwa ndani kisha nikaanza kuusafisha kwa vile ulikuwa umekaa siku nyingi bila kuutumia.
Ili kuupa uhai, niliuzungushia unga wa sembe na kuanza kuutabania maneno ya kichawi ambayo nilifundishwa na babu yangu aliponikabidhi mkoba huo.
Wakati wa kufanya kazi hiyo nilitakiwa niwe uchi. Hivyo nilikuwa nimevua bukta niliyokuwa nimevaa na kubaki uchi wa mnyama.
Baada ya kukamilisha ada ya mkoba huo, nilianza kuvirudisha vile vitu ndani ya mkoba. Kuvirudisha vile vitu pia kulikuwa na namna yake.
Unatakiwa uchuchumae kisha kile kitu unachokirudisha unaanza kukizungusha upande wa mgongoni kwako kutoka upande wa kulia kwenda upande wa kushoto na huko ndiko unakitia kwenye mkoba.