The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-13

0

ILIPOISHIA WIKIENDA

 Baada ya kukamilisha ada ya mkoba huo nilianza kuvirudisha vile vitu ndani ya mkoba. Kuvirudisha vile vitu pia kulikuwa na namna yake.

 Unatakiwa uchuchumae kisha kile kitu unachokirudisha unaanza kukizungusha upande wa mgongoni kwako kutoka upande wa kulia kwenda upande wa kushoto na huko ndiko unakitia kwenye  mkoba. SASA ENDELEA….

Nikawa nafaya hivyo. Wakati nimeshika ule mkono wa mtoto mchanga uliokuwa umekaushwa nikasikia sauti ikiniuliza:

 “Mume wangu unafanya nini?”

 Nikashtuka na kugeuza uso wangu. Nikamuona mke wangu amesimama katikati ya mlango akinitazama. Bila shaka aliamka kitandani na kujikuta yuko peke yake, hivyo akatoka uani kunitafuta.

 Mori wote wa uchawi uliokuwa umenipanda ukanishuka hapo hapo. Kwa kweli nilitahayari na kujisikia vibaya. Sikutaka mke wangu aone mambo yale kwa sababu si tu angeshtuka na kupata hofu bali pia angeanza kuwa na mashaka na mimi.

 “Mume wangu unafanya nini?” Mke wangu akaniuliza tena akiwa amenitolea macho ya mshangao.

 “Hebu rudi ndani,” nikamwambia.

 Mke wangu akabaki palepale kwenye mlango akiwa amenikodolea macho. Nilijua kilichomshangaza ni vile kuniona niko uchi wa mnyama halafu nafanya mambo ya ajabu nikiwa nimechuchumaa.

Kwa haraka nikawahi kuutia ule mkono wa mtoto mchanga kwenye ule mkoba. Niliona bora aone vitu vingine lakini asiuone ule mkono ambao nilijua ungemshtua sana.

 “Si nimekwambia rudi ndani?” Sasa nilimwambia kwa ukali kidogo baada ya kuona ameendelea kusimama akinitazama.

 Mke wangu alitii akarudi ndani. Nilimaliza kuvitia haraka haraka vile vitu vilivyobaki nikavaa bukta yangu.

 Niliuchukua ule mkoba wangu nikauficha sehemu fulani kule uani kisha nikarudi ndani.

 Mke wangu alikuwa amekaa kitandani akinisubiri.

 “Ulikuwa unafanya nini mume wangu?” akaniuliza kwa hofu.

Nikakaa kando yake.

 “Kuna kitu sikukuambia mke wangu. Kuna waziri mwenzangu alinipeleka kwa mganga leo, ndiyo nikaambiwa nifanye vile,” nikamdanganya.

 “Ulikwenda kwa mganga kwa ajili gani?” mke wangu akaniuliza akiwa amekunja uso kama vile nilimueleza kitu cha kinyaa.

 “Si kipindi cha bajeti hiki. Bila kuhangaika bajeti ya wizara yangu inaweza kukwamishwa na wabunge.”

 “Yaani una imani kweli kwamba uganga unaweza kusaidia bajeti yako ipite?”

 Ilikuwa wazi kuwa mke wangu alishaniona mimi mpuuzi.

 “Mimi siamini lakini kuna waziri mwenzangu ndiye aliyenishawishi. Aliniambia kikifika kipindi hiki mawaziri wengi wanakwenda kwa waganga. Mimi niliona niende tu lakini sina wasiwasi sana,” nilimjibu hivyo baada ya kuona sikuwa na jibu lakini nilijua fika kuwa nilijibu ujinga.

“Unakuwa kama hujiamini. Mimi sioni kama uganga unaweza kusaidia.”

“Ni kweli. Mimi mwenyewe pia nimeona ni upuuzi mtupu.”

 “Unajua umenishtua sana nilipoona umevua nguo uani. Huyo mganga ndiye aliyekwambia uvue nguo?”

 “Basi tuyaache mke wangu. Ni ujinga mtupu. Hebu tulale, kesho nahitajika kuamka mapema, nina kazi nyingi za kufanya ofisini.”

 Tukalala lakini mimi sikulala usingizi. Nilikuwa namtegea mke wangu apitiwe na usingizi ili nitoke tena. Katika kumsubirisha mke wangu alale, nikapitiwa mimi na usingizi.

 Nikiwa usingizini niliuona ule mkoba umeota mikono na miguu kama ya nzi ukinitambaa kwenye uso wangu. Nikagutuka.

 Nikaupangusa uso wangu uliokuwa ukitambaliwa kisha nikamchunguza mke wangu. Nikaona alikuwa amelala usingizi. Nikainuka na kutoka uani. Niliuchukua ule mkoba na kuja kuuweka chini ya mvungu wa kitanda.

 Ile ndoto niliyoota ilitokana na kuuweka ule mkoba              mahali pasipostahili kuwekwa. Ndiyo sababu niliona umeota miguu ukinitambalia usoni.

 Baada ya kuuweka mkoba huo nikalala tena. Usingizi ulinipitia mpaka asubuhi. Mke wangu ndiye aliyeniamsha.

 “Meshack! Meshack! Amka!” niliisikia sauti yake kwa mbali. Nikazinduka usingizini.

 “Nini?” nikamuuliza.

 “Si ulisema unataka kuamka mapema uwahi kazini, mbona bado umelala?” akaniambia.

 “Ni saa ngapi sasa?”

 “Saa kumi na mbili kasorobo.”

 Nikatenga shuka na  kuinuka. Nilikwenda maliwatoni. Nilitumia kama dakika thelathini kupiga mswaki, kuoga na kutoka bafuni.

 Nikatumia dakika nyingine zisizopungua kumi kuvaa. Nikachukua mkoba wangu wa ofisini na kumuaga mke wangu.

 Nilifika kazini kwangu dakika chache kabla ya saa moja asubuhi. Ilikuwa ni muhimu kuwahi kufika kazini kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya bajeti ya wizara yangu ambayo ilihitajika kusomwa bungeni siku mbili baada ya siku ile.

 Ninamaanisha kuwa siku ambayo ingefuata ningekwenda Dodoma ambapo ningelala siku moja na asubuhi itakayofuata niamkie bungeni.

 Nilikuta maafisa wa wizara yangu tayari walishafika wakiendelea na kazi.

 Siku ile tulishinda ofisini hadi saa kumi na moja jioni ambapo hutuba ya bajeti yangu ilikuwa imeshachapwa.

 Niliporudi nyumbani niliondoka nayo ikiwa kwenye mkoba wangu.

 Asubuhi ya siku iliyofuata nilimuaga mke wangu nikaanza safari ya kuelekea Dodoma. Ule mkoba wangu wa uchawi niliondoka nao.

Kwa vile tulikuwa tunasafiri kwa mwendo wa taratibu huku nikisoma hotuba yangu ya bajeti ndani ya gari, tulifika Dodoma jioni.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu. 

Leave A Reply