The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-13

0

ILIPOISHIA WIKIENDA:

Siku ile nilikunywa chai saa tano tena kwa kuhimizwa na mke wangu aliyekuwa Dar ambaye nilikuwa nikiwasiliana naye wakati wote. Kama si yeye kunihimiza, nilishausahau utaratibu wa kunywa chai asubuhi kutokana na kihoro nilichokuwa nacho.

SASA ENDELEA…

Zoezi la upigaji kura likaisha salama katika jimbo langu, japokuwa kulikuwa na dosari ndogondogo zilizokuwa zimejitokeza.

Sasa ikaanza kazi ya kuhesabu kura za udiwani, ubunge na urais.

Nilipokutana na marafiki zangu nilijipa moyo kwa kuwaambia kuwa nitashinda lakini moyoni mwangu sikuwa na uhakika wa kushinda.

Siku ile kura ziliendelea kuhesabiwa kwenye vituo hadi saa nne usiku. Matokea ya kura za udiwani yalifahamika usiku huohuo. Chama chetu kilikuwa kimezoa viti vingi vya udiwani. Matokea hayo kidogo yalinipa moyo.

Nilijiambia aliyempigia diwani wa chama changu, kama ana akili timamu, atakuwa amenipigia na mimi mbunge.

Siku ile sikulala kwa kufuatilia matokeo. Asubuhi kulipokucha kulikuwa na majumuisho ya kura zilizopigwa kutoka sehemu tofauti za Jimbo la Nzega.

Ilikuwa saa nane mchana, matokeo yalipokamilika na mshindi kufahamika. Bila kuamini masikio yangu, nilitangazwa kuwa mshindi wa kiti cha ubunge wa Jimbo la Nzega.

Hapohapo nikampigia simu mke wangu ili nimjulishe matokeo hayo.

Yeye alipopokea simu aliniuliza.

“Haya vipi huko? Matokeo bado tu?”

“Matokeo tayari,” nikamwambia bila kufafanua.

“Umeshinda?”

“Kwa nini nisishinde?”

“Sema kweli. Umeshinda Meshack?”

“Nimeshinda.”

“Mume wangu sasa ni mbunge!” Mke wangu akaanza kushereheka.

“Naam mume wako sasa ni mheshimiwa.”

“Basi nakuja nikusindikize Dodoma.”

“Unadhani kazini kwako watakupa ruhusa?”

“Kwa kweli sidhani.”

“Haina haja uje. Tutakuwa tunawasiliana kwenye simu.”

 “Basi utanijulisha mambo yanavyoendelea.”

“Usijali.”

Siku ile ilikuwa ni furaha tu, kwani hadi inafika saa kumi jioni, mgombea urais wa chama changu naye akatangazwa kupata ushindi wa kishindo dhidi ya wapinzani wake kutoka vyama vya upinzani.

Niligharamia vikundi kadhaa vya ngoma mitaani kusheherekea ushindi wangu. Kuna vikundi vingine vilikuwa kwenye magari vikitumbuiza huku gari likizunguka kila mtaa.

Vijana wa pikipiki ndiyo usiseme, walikuwa wamefanya maandamano wakizunguka mitaani huku wakipeperusha bendera ya chama chetu.

Ilimradi siku ile ilikuwa ya shangwe na hoihoi na pia ilikuwa siku ya hasara kwangu kwani kila nilipoishiwa na pesa niliingia ATM kutoa zingine.

Mara kwa mara mke wangu alikuwa akinipigia simu akitaka kujua mambo yalivyokuwa yakiendelea. Nilimweleza kuhusu sherehe zilizokuwa zinaendelea mitaani.

“Chama changu pia kimeandaa sherehe maalum ya kunipongeza mimi na mheshimiwa rais itakayoanza saa mbili usiku leo,” nikamwambia.

“Natamani ningekuwepo.”

“Usijali. Hivi ni vijimambo tu vinapita. Mambo ni bungeni.”

“Nakutakia heri mume wangu.”

“Asante sana.”

Wakati huo tayari nilikuwa nimeshapata marafiki wengi. Walikuwepo ambao walinisaidia kipesa kwani bila msaada wa watu wengine ningeliishiwa na pesa.

Siku niliyokwenda bungeni, mke wangu alifika Nzega. Chama changu kilitoa basi zima ili mashabiki wangu waweze kunisindikiza Dodoma. Nilifurahi kuwa katika msafara huo ambao mke wangu naye alikuwepo.

Tulifika Dodoma jioni, tukalala gesti. Kisheria nilitakiwa nilale hotelini kwa vile tayari nilishakuwa mheshimiwa lakini kwa siku ile ambayo nilikuwa sijaapishwa kuwa mbunge niliona nisingeweza kuwaacha mashabiki wangu walale gesti, mimi nikalale hotelini. Haukuwa uungwana.

Asubuhi yake walinisindikiza katika viwanja vya bunge ambako nilikutana na wabunge wenzangu mbalimbali ambao walitoka katika majimbo yao.

Baada ya kuapishwa, tukawa kwenye semina za kufundishwa juu ya sheria na kanuni za bunge.

Jambo ambalo sikulitarajia ni taarifa niliyoipata nikiwa bungeni kuwa rais alinitangaza kuwa mmoja wa mawaziri wake katika baraza lake la mawaziri aliloliunda mara tu baada ya kuapishwa kuwa rais.

Nikawa kwenye sherehe nyingine ya kuteuliwa kuwa waziri. Sikuwa peke yangu, karibu wote tulioteuliwa uwaziri tulikuwa tupo bungeni.

Sasa heshima yangu haikuwa ya ubunge pekee, ilikuwa ya ubunge na uwazi                                       ri. Sitapenda kutaja nilikuwa waziri wa wizara gani lakini ilikuwa wizara nyeti. Sikuweza kujua rais alifikiri nini mpaka akaamua kuniteua mimi kushika wizara ile.

Asubuhi ya siku iliyofuata nikawa Dar kwenye viwanja vya ikulu mimi na mawaziri wenzangu kwa ajili ya kuapiswa.

Baada ya kula kiapo cha kulinda katiba, kutekeleza majukumu yangu kwa uaminifu na kutotoa siri za serikali nje, nikaanza kazi.

Kila mmoja wetu alikuwa amekabidhiwa gari lake, alipewa kiasi cha pesa kwa ajili ya kununua suti za uwaziri na mahitaji mengine muhimu na pia alipewa nyumba ya kuishi.

Je, nini kiliendelea? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu. 

Leave A Reply