The House of Favourite Newspapers

Waziri alipokiri kuwa mchawi-14

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
Siku ile tulishinda ofisini hadi saa kumi na moja jioni ambapo hotuba ya bajeti yangu ilikuwa imeshachapwa.
Niliporudi nyumbani niliondoka nayo ikiwa kwenye mkoba wangu.
Asubuhi ya siku iliyofuata nilimuaga mke wangu nikaanza safari ya kuelekea Dodoma. Ule mkoba wangu wa uchawi niliondoka nao.
SASA ENDELEA…

Kwa vile tulikuwa tunasafiri kwa mwendo wa taratibu huku nikisoma hotuba yangu ya bajeti ndani ya gari, tulifika Dodoma jioni.
Nilifikia katika hoteli ambayo nilikodiwa chumba, nikapumzika kidogo baada ya safari ndefu ya kutoka Dar.

Si tu nilikuwa nimejiandaa kwa ajili ya hotuba ya bajeti ya wizara yangu ambayo ningeisoma bungeni kutakapokucha, bali pia nilikuwa nimejiandaa kwenda bungeni usiku ule kuliwangia bunge ili bajeti yangu iweze kupita bila matatizo.
Baada ya kula chakula cha usiku, niliingia chumbani mwangu na kuanza kupanga vifaa vyangu vya kazi kutoka katika mkoba wangu wa uchawi.

Niliendelea na ile kazi hadi saa saba usiku ambapo nilisubiri saa nane ifike. Huo ndiyo muda muafaka niliokuwa nimepanga nitoke.Dakika chache kabla ya saa nane, nikaanza kujipaka dawa zangu. Nilijipaka mwilini aina ya mavumba ya uchawi. Kutokana na mavumba hayo kufanana na masizi, uso wangu ulionekana mweusi kama kinyago cha mpapure.

Nikajifunga rubega kaniki yangu mpya niliyoinunua Dar es Salaam.
Nilitoka pale hotelini nikiwa na mkoba wangu begani, hakukuwa na mtu yeyote aliyeona wala kujua kwa sababu nilitoka kiuchawi. Ile dawa niliyojipaka ilinisaidia nisionekane.
Nikaanza kutembea kuelekea katika eneo lenye majengo ya bunge. Nilitembea kwa miguu lakini kwa vile nilikuwa nikitembea kiuchawi mwendo huo ulikuwa mfupi sana.

Nilifika katika majengo ya bunge dakika chache kabla ya saa tisa.
Nilikuta askari wakiwa katika geti la kuingilia lakini hawakuniona. Nikalizunguka jengo hilo huku nikitabana maneno ya kichawi.

Nilipotokea tena pale kwenye geti niliwapulizia mavumba wale askari nikiwa mbali kidogo na wao. Baada ya muda kidogo askari wote wakalala usingizi kabisa.
Nikaenda kufungua geti na kuingia. Kaniki yangu niliiacha kando ya geti hilo, nikabaki mtupu. Nikaanza kuwanga kuelekea katika mlango mkuu wa jengo la bunge huku nikimwaga mavumba ya kichawi.

Nilizunguka hapo mara saba kisha nikarudi kwenye geti na kukita kimba la kinyesi kabla ya kuvaa kaniki yangu na kutoka.

Niliwaacha wale askari wakiwa bado wamelala, nikaenda zangu. Wakati ninarudi hotelini nilijiridhisha kuwa nilichofanya kitasaidia kuwafanya wabunge wanikubali, waridhie hotuba yangu na waipitishe bila kupingwa.

Kwa vile wabunge wote hutumia mlango ule, hivyo kila atakayepita katika eneo lile ambalo nililimwagia mavumba atauvaa uchawi wangu.

Niliporudi hotelini, nililala kidogo kisha nikaamka. Haikuwa rahisi kupata usingizi mzuri kwa sababu ya wasiwasi niliokuwa nao. Nilikuwa na wasiwasi mwingi.
Muda ule kama ningelala sana ningechelewa kuamka. Isitoshe ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kwenda kusoma hotuba ya bajeti katika bunge hilo nikiwa waziri.

Lakini pamoja na uchawi nilioufanya bado nilikuwa na wasiwasi. Sikujua nini kingetokea kwani dawa zangu zingeweza kuzidiwa nguvu na za wenzangu. Wakati ninawanga katika eneo lile la bunge niligundua kulikuwa na ishara ya kuwepo na wenzangu waliozika dawa zao wakiwa na madhumuni kama yangu.

Hutokea zile dawa zikazidiana nguvu na upo uwezekano wa dawa zangu kushindwa kwa vile uchawi nilioutumia ulikuwa mwepesi. Inawezekana wenzangu wengine walitumia uchawi wa kutoa makafara.

Nilipoamka nilikwenda kuoga kisha nikavaa suti yangu ya kuingilia bungeni.
Nikahakiki mafaili yangu kwa mara ya mwisho na kuyapanga kwenye mkoba wangu kisha nikatoka.

Dereva wangu alikuwa akinisubiri nje ya hoteli. Nikajipakia kwenye gari, tukaondoka.
Nilipofika bungeni mazungumzo yaliyokuwepo ni ya kukutwa kwa kinyesi cha binadamu kando ya geti la kuingilia bungeni.

Kinyesi hicho kiligunduliwa asubuhi na haikufahamika kiliachwa na nani licha ya kuwepo askari kwenye geti la bunge.Niliambiwa kwamba askari hao walikuwa wanahojiwa kuhusiana na suala hilo.

Leave A Reply