The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-16

0

ILIPOISHIA IJUMAA:
Baada ya hotuba yangu ndefu nilitaka kusikiliza kero za wananchi. Wananchi mbalimbali walijitokeza na kutoa kero zao na niliahidi kuzishughulikia.

Jambo ambalo lilinishtua kuliibuka kundi la akina Mzee Mgorozi na Bi Shali ambalo lilinishutumu kuwa tangu nilipopata ubunge nilikuwa nimewasahau na nilikuwa sifiki kijijini kwetu.

Walinitolea maneno mengi ya kashfa hadi polisi wakalazimika kuwaamuru waondoke. Wazee hao wachawi hawakutaka kuondoka. Waliwaambia polisi kuwa mimi ni mwenzao na kwamba tunajuana tulikotoka.

Nikaona wale wazee wanataka kuniadhiri. Bi Shali aliniuliza ni kwa nini nilifika Nzega tangu jana lakini sikufika kijijini kwetu kuwaona?
Sikuwa na jibu. Kwa vile walikuwa wananitolea kashfa nikawaagiza polisi wawaondoe kwa nguvu.

Wakati wazee hao wanaondolewa, Mzee Mgorozi alininyooshea kidole na kuniambia.
“Wewe mchawi mkubwa. Ulipata ubunge na uwaziri kwa sababu ya uchawi. Na sisi ndiyo tuliokusaidia.” SASA ENDELEA…

“Na bado tunakudai, hujalipa deni letu,” Bi Shali akaongeza.
Nilipoona watu waliokuwa wanawasikiliza wangeweza kugundua kitu, nikawaonesha polisi ishara ya mkono kuwa wawaondoe haraka watu hao.

Kwa vile walileta ubishi, walikokotwa kwa nguvu na polisi na kupakiwa kwenye gari la polisi. Gari hilo likaondoka na watu hao. Bila shaka walipelekwa kituo cha polisi.
Ingawa walichosema kilikuwa na ukweli lakini kitendo cha kunivamia kwenye mkutano na kuleta maneno ya kashfa hakikustahili.

Nikajiambia: “Potelea mbali, nawapelekwe tu.”
Nilipomaliza mkutano wangu nilirudi hotelini ambako nilikuwa nimekodi chumba huku nikiwa na fadhaa. Vitendo vya Mzee Mgorozi na Bi Shali vilikuwa vimenikera sana.
Baadhi ya watu wangeweza kuwahisi ni wendawazimu lakini watu wengine wangeweza kuamini kuwa mimi ni mchawi na nilipata ubunge wangu kwa njia za uchawi. Nilihisi jambo hilo lingeweza kupunguza imani ya wapiga kura wangu juu yangu.

Kama ambaye nilijua kuwa wazee hao wangeweza kuniletea matatizo, nilipofika Nzega sikutaka kwenda kule kijijini na sababu kubwa ni kuwa sikutaka kukutana na wazee hao. Sikujua ni nani aliwaambia kuwa nimekuja hadi wakanifuata pale kwenye mkutano.

Nikiwa hapo hotelini, majira ya saa nne usiku, mkuu wa polisi wa Wilaya ya Nzega alinipigia simu na kuniambia kuwa wale wazee waliokamatwa kwenye mkutano wangu watafikishwa mahakamani kesho yake.

“Mtawashtaki kwa kosa gani?” nikawauliza.
“Kosa la kuleta vurugu kwenye mkutano na kutoa maneno ya kashfa dhidi yako.”
Nilitaka kumwambia afisa huyo wa polisi awaachie lakini nilisita. Nilihisi nikimwambia hivyo hatanielewa au ataona ni kweli nilikuwa na uhusiano nao. Nikamwambia.
“Sawa.”

Moyoni mwangu nilijiambia, waliyataka wenyewe, shauri zao.
Usiku ule nilipokuwa nimelala nilipata hofu kwamba wachawi wenzao wangeweza kunifuata humo chumbani na kuniletea tafrani kutokana na wenzao kukamatwa lakini nililala hadi asubuhi bila kuona tatizo lolote.

Wakati napata kifungua kinywa asubuhi, nilipigiwa simu tena na afisa wa polisi wa wilaya na kunieleza mkasa wa ajabu.Aliniambia usiku uliopita majira ya saa nane usiku, polisi wawili waliokuwa wamebaki kaunta walimuona paka mweusi akiingia ndani ya kituo hicho. Walitaka kumchunguza lakini baadaye aliwapotea.

Baada ya muda kidogo, walimuona paka huyo akiwa na paka wenzake watatu wa rangi tofauti wakitokea upande wa mahabusu na kutoka kwenye lango la kituo cha polisi.
Polisi hao walishtuka na kuwafuatilia nje ya kituo, wakawaona wakienda zao pembeni mwa barabara wakiwa wamefuatana.

Jambo hilo liliwashangaza sana. Polisi hao wakarudi ndani ya kituo na kwenda upande wa mahabusu walikotoka paka hao ili kujua walitokea wapi.

Walipochungulia ndani ya chumba cha mahabusu ambamo wale wazee wachawi walikuwa wamefungwa, hawakuona mtu yeyote.

Leave A Reply