Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-41

ILIPOISHIA IJUMAA:
Mheshimiwa waziri badala ya kuvishika vitu hivyo kwa mkono alikwenda kuvaa soksi mikononi kisha akavikusanya kwenye gazeti. Niliamini kuwa sasa alikuwa akiviona vitu vyake hivyo ni kama najisi.
Baada ya kuvikusanya kwenye gazeti alikwenda kuvimwaga uani, akavinyunyizia mafuta ya petroli kisha akaviwasha.

Mkoba huo wa kichawi uliteketea kabisa.
Tuliporudi ndani nikamwambia ampigie simu mke wake amuite.
Waziri alisita kidogo lakini baadaye alitoa simu yake akampigia mke wake. Wakati simu yake inaita alinipa.

“Naomba uzungumze naye wewe, mimi hawezi kunielewa.”
Nikapokea ile simu na kuiweka karibu na sikio langu. Mke wake alipopokea simu nilijitambulisha kwake kisha nikamwambia aje pale nyumbani na mtoto.
SASA ENDELEA…

“Mheshimiwa waziri pia yupo hapo?” mwanamke huyo akaniuliza.
“Ndiyo yupo.”
“Haya ninakuja.”
“Ufike sasa hivi, tunakusubiri.”
“Sawa tunakuja.”

“Kwa nini hukutaka kuzungumza naye wewe?” nikamuuliza waziri mara tu nilipokata simu.
“Akisikia kwamba unamuita wewe inampa uzito zaidi wa kuja, ningemuita mimi tungeanza kubishana na kuulizana maswali. Mke wangu hana imani tena na mimi kutokana na mambo ambayo nimekueleza.”
“Nitayatatua matatizo yenu na ninaamini kuwa yatakwisha.”

“Nitashukuru sana kwa sababu hili suala limenitesa sana hasa kwa upande wa mtoto wetu.”
Baada ya nusu saa tu, mwanamke huyo pamoja na mtoto wake wakawasili.
Waliingia sebuleni tulipokuwa tumekaa, akatusalimia sote kisha akaketi.
“Unamuonaje mtoto?” nikamuuliza.

“Mtoto anaumwa. Leo nilishindwa kufika kanisani kwa sababu nilimpeleka hospitali.”
“Alianza kuumwa tangu lini?”

“Karibu wiki nzima hii lakini alikuwa amepata nafuu kidogo, jana usiku ndipo alipozidiwa.”
“Nini kilimtokea jana usiku?”
Pamoja na kumuuliza hivyo, sababu nilishaifahamu baada ya mheshimiwa waziri kunieleza ila nilimuuliza ili kujua undani wake.

“Kuna wachawi wanakuja nyumbani usiku karibu wiki nzima hii. Wanataka wamchukue huyu mtoto….”
Ilikuwa kama niliyemchokoza mwanamke huyo kwani alinieleza mkasa mzima tangu wachawi hao walivyoanza kuwafuata nyumbani usiku hadi alipohamia kwao ambapo jana yake walirudi tena usiku.
Habari ile haikuwa ngeni kwangu kwani mheshimiwa waziri alishanieleza. Hivyo mwanamke huyo aliponieleza tena haikunishtusha.

Alipomaliza kunieleza mkasa huo mwanamke huyo ambaye alikuja akiwa na uso mkunjufu alianza kutokwa na machozi.

“Hebu mlete huyo mtoto,” nikamwambia mke wa waziri ambaye alinipa mtoto huyo.
Wakati namshika nilikuta mwili wake ulikuwa wa moto na alikuwa amelegea sana.
“Ana moto sana na anaonekana kama amechoka.”
“Huo moto ni tangu jana usiku walipokuja wale wachawi.”
“Hospitalini walikuambia ana nini?”

“Safari hii walipompima waliniambia hawakuona ugonjwa wowote ni uchawi tu.”
“Hospitalini walikuambia ni uchawi tu?” nikamuuliza baada ya kutomuelewa.
“Hivyo nasema mimi kwa sababu wale watu wanapoanza kuja ndiyo mtoto anaanza kuumwa.”
Nikakishika kichwa cha yule mtoto na kumuombea. Nilimuombea sana kisha nilimuombea mama yake.
Nilipomaliza nilimwambia mwanamke huyo.

“Mume wako amenieleza kila kitu. Matatizo yote yameanzia kwa babu yake na yeye akajikuta ameingia katika mkumbo ambao hakuweza kuuepuka. Ule mkoba uliowaletea matatizo nimeshauteketeza kwa moto, haupo tena na yeye mwenyewe ni kama aliyezaliwa upya. Mtu unapotubu makosa na kuamua kuwa katika mstari, unakuwa kama uliyezaliwa upya na hivyo ndivyo alivyo mume wako kwa sasa.”
Baada kumwambia hivyo nilimuuliza.

“Umerudisha imani kwa mume wako?”
“Mpaka anihakikishie kuwa mwanangu atakuwa salama.”
“Ninakuhakikishia mimi kuwa hakutakuja wachawi wowote watakaomchukua mwanao.”
“Kama hawatakuja tena na ule mkoba wake ameutoa, nitarudisha imani kwake.”
“Utarudi nyumbani kwake?”

“Kwa amri yako wewe mchungaji nitarudi.”
“Nawaomba mpeane mikono, mrudishe amani, muaminiane na mpendane kama mlivyokuwa zamani.”
Hapo nikamuona mke wa waziri akimgeukia mume wake na kumpa mkono. Nikamuona waziri aliyekuwa amekata tamaa akitabasamu.

“Nakuomba uniamini mke wangu, urudishe amani na upendo,” waziri akamwambia mke wake.
“Kutoka sasa ninakuamini na nitarudisha amani iliyokuwa imepotea.”
“Kitu kimoja hujataja,” nikamkumbushia mwanamke huyo.
“Kitu gani?” akaniuliza.

“Upendo.”
Wote wawili wakatabasamu.
“Samahani mchungaji nilisahau. Nitamuamini mume wangu na nitarudisha amani na upendo.”
“Na Mungu atawabariki,” nikawaambia.

Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Loading...

Toa comment