visa

Waziri alipokiri kuwa mchawi-8

ILIPOISHIA IJUMAA:
Siku moja kabla sijarudi Dar kuendelea na masomo yangu ya chuo kikuu, wazee hao pamoja na babu waliniweka kikao usiku. SASA ENDELEA…

Wazee hao waliniambia kuwa nina deni lao na kila nitakapokwenda nilikumbuke deni hilo.
Hilo deni nilikuwa nalijua. Babu alishanieleza kwamba nilitakiwa nioe mke ili mtoto wangu wa kwanza nimtoe kafara kwa wachawi hao.Wakati ule nakumbushwa deni hilo nilikuwa nimeshakula makafara mawili ya wenzangu waliotoa watu wao.

“Hilo deni nalijua lakini ni mpaka nimalize masomo yangu,” nikawaambia.
“Tunakukumbusha tu na mimi nataka niwe hai hadi muda huo nionje nyama ya mwanao,” Bi Shali akaniambia.

“Yeye ameshakula nyama za wenzake mara mbili na sisi tunangoja kafara lake,” Mzee Mgorozi akadakia.
“Babu amenisisitiza sana. Hilo ninalijua. Msiwe na wasiwasi,” nikawaambia.
“Kwanza baba yako alikufa na deni letu, hakutoa kitu. Sisi tulitaka kukuchukua wewe lakini babu yako alikataa,” Bi Shali akaniambia.

“Ngojeni nioe mke, nikimaliza masomo tu naoa. Mtoto wangu wa kwanza nawapa.”
“Usisahau ahadi yako bwana mdogo,” Mzee Maziku aliyekuwa kimya muda wote akanisisitizia.
Binadamu walikuwa na uchu wa kula nyama ya binadamu mwenzao kama wanyama. Babu yangu aliwahi kuniambia ukitaka kuwa mchawi na uchawi ukukubali ni lazima ujigeuze roho yako uwe kama mnyama.

Kwa nje utaonekana kama binadamu lakini kwa ndani yako unakuwa sawa na mnyama.
Nilipomuuliza babu ni kwa nini ukiwa mchawi unatakiwa uwe na moyo wa kinyama, aliniambia hapo ndipo uchawi utakapokukubali kwa sababu vitendo vya kichawi pia ni vya kinyama ikiwemo kula nyama za binadamu wenzako waliokufa.

Unapoanza sasa kujiingiza katika vikundi vya wachawi, utaona uchawi unachosha, lakini taratibu unaanza kuzoea na ghafla unajikuta ukifurahia kula nyama ya ndugu yako aliyekufa.

Na kama unakula nyama ya maiti, unatakiwa ule nyama ya mtu anayekuhusu sana kama vile mwanao, mkeo au ndugu yako ili kuukamilisha unyama wako. Nyama ya mtu baki haitakiwi.

Ndiyo maana kunakuwa na ada ya kila mwanauchawi kutoa mtu anayemhusu ili aliwe na hii ni kila baada ya kipindi fulani. Usipotoa mtu unabaki na deni. Na kuna siku mtu wako anaweza kuchukuliwa kinguvu na wachawi wenzako kulipa deni lao. Wanasheria za kutisha sana!

Baada ya kuweka makubaliano na wale wazee wachawi, nilirudi Dar kuendelea na masomo. Kusema kweli nilipenda niwe mchawi na nilidhamiria kumtoa mwanangu wa kwanza aliwe ili nilipe deni la marehemu baba yangu na deni langu mimi mwenyewe.

Niliona umuhimu wa kumtoa mwanangu kwa kuzingatia kuwa wachawi walitaka kunichukua mimi kufidia deni la baba. Kama si babu yangu kunitetea, ningelikwisha kuwa matumboni mwao siku nyingi. Masomo ya chuo kikuu nisingeyapata.

Baada ya kumaliza masomo yangu ya chuo kikuu nilipata ajira Wizara ya Mambo ya Ndani. Nilifanya kazi kwa mwaka mmoja. Palepale wizarani nikapata msichana ambaye nilimpenda tukafunga uchumba.
Nilipopata likizo nilirudi kijijini kwetu na kumjulisha babu yangu kuwa nimepata mchumba.

“Nasumbuliwa sana na Bi Shali kuhusu suala lako. Wanaona kama umewageuka,” babu akaniambia.
“Hapana babu sijawageuka. Mimi bado ni mwenzao na naikumbuka ahadi yangu.”
“Sasa utakuja uwanjani leo?”

“Waambie nitakuja na tutaonana. Nataka niongeze nguvu. Pale wizarani nilipo sitaki mtu anichezee.”
“Basi njoo upewe miti ya kichawi. Tukutengenezee mfuko wako uende nao Dar.”

Usiku wa siku ile nilienda na babu kule kiwanjani. Wale wazee wachawi waliponiona walifurahi kwani nilikuwa nimejifunga kaniki mpya. Wakaona pamoja na usomi wangu bado nilikuwa mwenzao.
Bi Shali akaniambia ameona ishara kuwa ninakaribia kuoa. Nikashtuka sana kwa sababu sikuwaambia kuwa nilikuwa na mpango huo.

Nikaona nimkubalie.
“Na unaikumbuka ahadi yetu?” akaniuliza.
“Naikumbuka vizuri.”

“Kama unaikumbuka hakuna tatizo, sisi tunakutakia mema.”
Niliendelea kushirikiana na wale wachawi mpaka likizo yangu ilipomalizika nikarudi Dar.
Baada ya miezi mitatu tu nikafunga ndoa na Suzana, msichana niliyekuwa ninafanyanaye kazi. Lakini mwezi uleule nikapata habari kuwa babu yangu alikuwa mgonjwa sana.
Toa comment