The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-9

0

ILIPOISHIA WIKIENDA

Usiku wa siku ile nilienda na babu kule kiwanjani. Wale wazee wachawi waliponiona walifurahi kwani nilikuwa nimejifunga kaniki mpya. Wakaona pamoja na usomi wangu bado nilikuwa mwenzao. 

Bi. Shali akaniambia ameona ishara kuwa ninakaribia kuoa. Nikashtuka sana kwa sababu sikuwaambia kuwa nilikuwa na mpango huo. 

Nikaona nimkubalie. 

“Na unaikumbuka ahadi yetu?” akaniuliza. 

“Naikumbuka vizuri.” 

“Kama unaikumbuka hakuna tatizo, sisi tunakutakia mema.”

 Niliendelea kushirikiana na wale wachawi mpaka likizo yangu ilipomalizika nikarudi Dar. SASA ENDELEA…

Baada ya miezi mitatu tu nikafunga ndoa na Suzana msichana niliyekuwa ninafanya kazi naye. Lakini mwezi uleule nikapata habari kuwa babu yangu alikuwa mgonjwa sana huko kijijini kwetu. Nikaomba ruhusa kazini kwangu na kwenda kumjulia hali.

Nilifika jioni. Nikakaa na babu chumbani kwa karibu saa mbili. Aliniambia:

“Babu naona kama sitapona tena, kila mara namuona baba yako ananiita.”

“Babu usiwaze hivyo, unaweza kupona. Kuugua siyo kufa.”

Babu hakuniambia kitu tena. Akabaki kunitazama huku akijaribu kutoa tabasamu ambalo sikuweza kujua lilikuwa ni la nini. Baada ya kimya kifupi akaniambia:

“Hebu angalia mvunguni mwa kitanda changu.”

Nikapiga magoti na kuchungulia chini ya mvungu wa kitanda alicholala.

“Umeona nini,” akaniuliza.

“Kuna kiza labda niwashe simu yangu nipate mwanga.”

“Hapana. Usiwashe kitu. Tia mkono upapase, utaona kitu.”

Nikatia mkono na kupapasa.

“Sioni kitu babu,” nikamwambia.

“Njoo upande huu wa kichwani kwangu.”

Nikasogea upande wa kichwani kwake. Nilipopapasa nikashika mfuko wa ngozi. Nikautoa. Ulikuwa ni ule mkoba wake wa uchawi.

“Kuna huu mkoba wako,” nikamwambia.

“Nipe.”

Nikampa. Aliushika kwa mikono miwili kisha akaniambia:

“Umefanya vizuri kuja hapa Mbogwe wakati huu.”

Akanipa ule mkoba.

“Nakukabidhi huu mkoba wangu uuendeleze na wewe utaukabidhi kwa mwanao au mjukuu wako muda wako utakapowadia.”

Wakati naupokea ule mkoba babu akafumba macho. Ikawa ndiyo safari!

Alikufa palepale.

Kifo cha babu kilinihuzunisha sana kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa kama baba yangu. Katika historia yangu baba na mama yangu walikufa nikiwa mdogo na hivyo nikalelewa na babu yangu ambaye naye mke wake alikwishakufa zamani.

Kwa hiyo nilikuwa nimemzoea babu na kumuona kama mzazi wangu hasa vile ambavyo wazazi wangu hawakuwepo. Kifo chake kilikuwa kama kitambulisho kuwa sasa nilikuwa nimebaki mwenyewe. Sina babu wala baba.

Lakini tayari nilikuwa mtu mzima mwenye elimu yangu na niliyekwishaanza kujitegemea mwenyewe. Nilimshukuru babu kwa kunilea na kunipa elimu. Hilo sijalisahau hadi leo.

Baada ya maziko ya babu yangu, mzee Mgorozi alinifuata akaniambia:

“Babu yako alikuwa mwenzetu sana lakini sasa ameshatutoka.”

“Ni kweli,” nikamwambia.

“Lakini hatujali sana kwa sababu wewe upo utashika nafasi yake.”

“Mimi nipo lakini ninaishi Dar.”

“Haijalishi unaishi wapi. Hata kama unaishi Dar, una maana huwezi kuja tena kijijini kwenu?”

“Nitakuja. Hapa ni kwetu, lazima nije.”

“Si unaikumbuka ile ahadi yetu?”

“Naikumbuka sana.”

“Usije ukaona babu yako amekufa ukajua na ile ahadi imekufa.”

“Ile ahadi ipo vilevile.”

Mzee Mgorozi akafurahi na kunipa mkono.

“Sasa kuna kitu kimoja nataka nikwambie.”

“Niambie.”

“Inabidi leo usiku tumchezee marehemu babu yako ngoma zetu za kichawi na wewe unatakiwa uwepo.”

“Kwani ni mpaka niwepo, mnaweza kucheza nyinyi.”

“Ni lazima uwepo, hizi ndizo kanuni zetu. Mbona unataka kuanza ubishi?”

“Hapana sitaki kuanza ubishi. Mimi kesho alfajiri naondoka kurudi Dar, sasa siwezi kukesha kwenye ngoma.”

“Unataka kuvunja miiko yetu?”

“Sivunji miiko, ninahitajika Dar.”

“Kwa nini usiende kesho mchana?”

“Nataka niwahi kazini. Ruhusa yangu imeisha tangu jana.”

“Mzee Mgorozi akaguna. Alionesha waziwazi kufadhaika. Kwa shingo upande akaniambia:

“Sawa bwana mdogo, nitawaambia wenzangu maneno yako.”

Nilikuwa sina mpango wa kuondoka alfajiri. Ningeondoka mchana.

Leave A Reply