Waziri aliyekuwa Mchawi-6

ILIPOISHIA IJUMAA:
Alipomaliza alitia mate kwenye viganja vyake akavisugua tena kisha akanipaka mimi usoni. Kwa vile babu alikuwa anakula ugoro, uso wangu ukawa unanuka ugoro.
“Babu unanipaka nini, mbona vinanuka sana?” nikamuuliza.

“Vinanuka? Visivyonuka ni vipi?” babu naye akaniuliza kwa kejeli.
“Vinanuka. Sijui ugoro, sijui vitu gani… !”
Kabla sijamaliza kusema nikapiga chafya.
“Afya,” babu akaniambia. Akaendelea.
SASA ENDELEA…

“Lazima nikupake hii dawa. Hii ndiyo itakayokutambusha tukifika kwa wenzetu.”
“Mbona ulipojipaka wewe hukutia mate yako?”
“Sasa acha kuuliza maswali yako, twende.”
Babu akanishika mkono na kuniongoza kuelekea kwenye njia ya kuelekea kwenye makaburi.
Halikuwa eneo kubwa sana ila lilikuwa na vichaka vingi pamoja na miti.

Katikati ya eneo hilo tulikuta watu wachache ambao walionekana kama walikuwa katika kikao fulani lakini walipotuona sisi wakanyamaza na kututazama.
Jumla walikuwa watu saba, wanaume wanne na wanawake watatu. Walikuwa wamesimama kando ya mti wa mkuyu. Wote walikuwa wamejifunga kaniki kama tulivyojifunga mimi na babu.

Kulikuwa na bibi mmoja kizee aliyekuwa na kibyongo. Alikuwa ameshika mwengo. Kaniki yake ilikuwa imechupa na kuchanika hivyo sehemu zake za siri zilikuwa wazi lakini hakuonekana kujali.
Alikuwa akiwazunguka wenzake huku akiwaputiaputia ule mwengo wake.

Babu alikwenda na mimi hadi kilipokuwa kile kikundi cha watu. Watu wote wakanikodolea macho na mimi nikawakodolea yangu. Wote niliwafahamu.

Baadhi yao walikuwa rafiki wa babu yangu. Mara kwa mara walikuwa wakija nyumbani. Yule bibi aliyekuwa ameshika mwengo alikuwa akiuza mbaazi karibu na shule ya msingi ya pale kijijini kwetu. Kumbe naye ni mchawi.

Siku ile niliwagundua wachawi wa kijijini kwetu. Niliona watu ambao sikuwadhania kabisa.
Mtu wa kwanza ambaye babu alimtambulisha kwangu alikuwa ni yule bibi. Alimwambia kwa kinyumbani kwamba, amekwenda kuniunganisha rasmi na kikundi chao.
“Haya karibu bwana mdogo.” Yule bibi akaniambia kisha akaipenua shuka niliyokuwa nimevaa na kunichungulia. Sijui alitaka kujua kama nilikuwa nimevaa kitu ndani.

Alipoona nilikuwa mtupu, akatingisha kichwa kuonesha ishara ya kunikubalia.
“Utakuwa unakuja hapa kila siku usiku saa kama hizi ukutane na wenzako,” akaniambia.
“Sawa,” nikamkubalia.

“Siri zetu hazitoki nje. Unayoyaona hapa yanabaki kuwa siri yako kwa maana wewe bado ni mdogo ni lazima nikutahadharishe.”
“Nimekuelewa bibi.”

“Babu yako amenifahamisha kuwa angekuleta leo. Nimekuandalia dawa yako maalum. Nitakuogesha na nitakunywesha hapahapa.”
“Sawa.”
Kazi yangu ilikuwa ni kukubali tu.

Yule bibi alikwenda kwenye shina la ule mti uliokuwa pale. Kulikuwa na kitu alichokichukua. Akarudi akiwa na kibuyu.
“Haya njoo huku,” akaniambia huku akiongoza njia kuelekea kwenye kaburi lililokuwa karibu yetu, akasimama katikati ya kaburi hilo.
Nikamfuata.

“Na ninyi njooni. Mbona mmesimama?” akawaambia wale watu wengine.
Watu hao pamoja na babu yangu wakaja kulizunguka lile kaburi. Mimi nilisimama katikati ya kaburi hilo pamoja na yule bibi.

“Vua shuka lako, nipe mimi,” yule bibi akaniambia.
Yule bibi aliponiona nasitasita, akaniambia.
“Hata mimi navua yangu.”

Akaivua ile kaniki aliyokuwa amevaa na kubaki uchi wa mnyama. Nilishindwa hata kumuangalia.
Ile methali ya ‘ukiyavulia nguo maji huna budi kuyaoga’ ikanijia akilini. Palepale nikavua kaniki na kumpa. Na mimi nikabaki uchi kama nilivyozaliwa.

“Nataka nisikie sauti zenu, leo tunamkaribisha mgeni,” sauti ya bibi ikasikika akiwaambia wale watu.
Hapohapo wakaanza kulizunguka lile kaburi huku wakiimba na kucheza ngoma ya kuinama na kurudi kinyumenyume.

Wakati huohuo yule bibi akawa ananimwagia dawa ya majimaji kutoka kwenye kile kibuyu. Alinimwagia kuanzia kichwani hadi miguuni.
Alipomaliza alinisogezea mdomo wa kile kibuyu kwenye mdomo wangu na kuniambia.
“Kunywa.”

Kwanza nilisita. Nikawa navuta harufu.
“Kunywa upate nguvu,” akaniambia.
Nikapiga funda moja. Ilikuwa dawa chungu kama shubiri.
“Meza unywe tena.”
Nikajikaza na kuimeza kisha nikapiga funda lingine. Nikalimeza harakaharaka.
“Kunywa tena.”
Nikapiga funda la tatu.

Nikaona yule bibi anakiondoa kile kibuyu midomoni mwangu.
Baada ya kumeza lile funda la tatu nilianza kuona mabadiliko mwilini mwangu na akilini mwangu.
Kwanza nilipovua ile kaniki nilikuwa nikisikia baridi kali lakini baada ya kumwagiwa ile dawa na nyingine kuinywa, nikawa nasikia joto. Pia nilipofika katika eneo lile nilikuwa muoga. Lakini ule uoga ukanitoka, nikawa jasiri kiasi kwamba ningeweza kubaki peke yangu pale makaburini hadi asubuhi.
“Unajionaje sasa?” Bibi akaniuliza.

“Najisikia niko jasiri sana,” nikamwambia.
Bibi akacheka. Alipofungua mdomo wake sikuona jino hata moja. Alikuwa kibogoyo kabisa.
Je, nini kiliendelea? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.


Loading...

Toa comment