Waziri Aliyekuwa Mchawi-7

ILIPOISHIA WIKIENDA

“Kunywa upate nguvu,” akaniambia. 

Nikapiga funda moja. Ilikuwa dawa chungu kama shubiri. 

“Meza unywe tena.” 

Nikajikaza na kuimeza kisha nikapiga funda lingine. Nikalimeza harakaharaka.

“Kunywa tena.” SASA ENDELEA…

Nikapiga funda la tatu.

Nikaona yule bibi anakiondoa kile kibuyu midomoni mwangu.

Baada ya kumeza lile funda la tatu nilianza kuona mabadiliko mwilini mwangu na akilini mwangu.

Kwanza nilipovua ile kaniki nilikuwa nikisikia baridi kali lakini baada ya kumwagiwa ile dawa na nyingine kuinywa nikawa nasikia joto.

Pia nilipofika katika eneo lile nilikuwa muoga. Lakini ule uoga ukanitoka nikawa jasiri kiasi kwamba ningeweza kubaki peke yangu pale makaburini hadi asubuhi.

“Unajionaje sasa?” Bibi akaniuliza.

“Najisikia niko jasiri sana,” nikamwambia.

Bibi akacheka. Alipofungua mdomo wake sikuona jino hata moja. Alikuwa kibogoyo kabisa.

“Unatakiwa uwe jasiri, uweze kukabiliana na kilichoko mbele yako,” bibi akaniambia.

“Kipi hicho?” nikamuuliza.

“Utakuja kukiona. Bado utakabiliwa na mitihani mingi ambayo ni lazima uishinde ili uwe gunge kama babu yako.”

Bibi sikumuelewa lakini sikutaka kumuuliza tena nikabaki kimya.

“Sasa turudini kulekule tukakuchezeshe ngoma,” bibi akawaambia wale watu.

Watu wote wakarudi chini ya ule mti. Yule bibi alikuwa amebaki mtupu vilevile. Jinsi alivyokonda mbavu zake zilikuwa zikionekana. Kifua chote alikuwa amekizungushia hirizi za rangi mbalimbali. Zilikuwepo nyekundu, nyeupe na nyeusi.

Tukakaa mduara na kucheza ngoma ambayo nilikuwa siielewi. Yule bibi ndiye aliyekuwa akituongoza na mwengo wake. Alikuwa akiimba na kucheza.

Kwa vile mimi ilikuwa ni mara ya kwanza kuchezeshwa ngoma ile, mara kwa mara yule bibi alikuwa akinielekeza jinsi ya kucheza.

Ngoma ilipovunjwa yule bibi akatoa hutuba fupi ya kututaka tufike tena kesho yake bila kukosa. Babu akatakiwa ahakikishe kuwa anafika na mimi.

Tuliporudi nyumbani nilimuuliza babu maswali mengi sana kuhusu yale yote niliyoyaona kule. Baadhi ya maswali alinijibu lakini mengine alishindwa kunijibu.

“Usiwe mdadisi sana. Mambo yote unayouliza utakuja kuyajua,” babu akaniambia.

Asubuhi kulipokucha nilichelewa sana kuamka kwa sababu usiku uliopita nililala kwa muda mfupi tu.

Nilipoamka ilikuwa karibu saa nne. Baada ya kuoga nilivaa nikanywa chai kisha nikatoka kwenda kumtembelea yule bibi mchawi anayeuza mbaazi zake jirani na shule ya msingi ya kijijini kwetu.

Nilikuta ameshaondoka. Nikafikiria niende nyumbani kwake lakini nikaona niachane naye.

Kutoka siku ile nikawa nimejiunga na kikundi kile cha wachawi. Kila usiku babu alikuwa ananipeleka makaburini ambako wachawi hukutanika kucheza ngoma za kichawi na kufanya mikutano yetu.

Tukirudi nyumbani babu naye alikuwa akinifundisha uchawi. Alikuwa akinipeleka maporini na kunionesha miti mbalimbali ya uchawi na kunieleza juu ya kazi zake.

Muda wangu wa kwenda masomoni ulipowadia nikaenda shule Tabora. Lakini wakati huo nilikuwa nimeshaanza kuujua uchawi.

Nilipomaliza kidato cha tano nilirudi kijijini kwetu na kuendelea na mafunzo yangu ya kichawi.

Mara kadhaa yule bibi alinichukua kwenda kuwachawia wafanyabiashara wakubwa wakubwa waliokuwa wakiishi Nzega.

Tulikuwa tunajigeuza paka na tunatembea kwa miguu kutoka kijijini kwetu hadi Nzega ambako tunakwenda kuwachawia watu hao kisha tunarudi wakati wa alfajiri.

Likizo yangu ilipomalizika nikarudi Tabora  kuendelea na masomo ya kidato cha sita.

Licha ya kujishirikisha na vitendo vya kichawi nilikuwa na akili ya masomo kiasi kwamba nilichaguliwa kwenda chuo kikuu kuendelea na masomo ya juu baada ya kumaliza kidato cha sita.

Nilipangiwa kwenda Chuo cha Mlimani jijini Dar. Kila nilipopata likizo nilikuwa ninarudi kijiini kwetu. Wale wazee waliposikia kuwa nimekuja walinifuata nyumbani.

Kulikuwa na wazee wanne waliokuwa msitari wa mbele kunifuatilia.

Kwanza alikuwa yule bibi ambaye baadaye nilifahamu jina lake alikuwa akiitwa Bi Shali. Halafu kulikuwa na mzee Mgorozi, mzee Maziku na mzee Nyagu.

Niliambiwa kuwa mzee Mgorozi ndiye aliyekuwa ameandaliwa kushika nafasi ya Bi Shali pindi atakapokufa.

Siku moja kabla sijarudi Dar kuendelea na masomo yangu ya chuo kikuu, wazee hao pamoja na babu waliniweka kikao usiku.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu. 

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

globalbreakingnews.JPG


Loading...

Toa comment