WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina leo Jumatano, Juni 20, 2018 ameliomba radhi Bunge kwa kitendo cha maofisa wa wizara yake kuingia kwenye mgahawa wa Bunge jijini Dodoma na kupima kwa rula samaki waliopikwa kwa ajili ya kitoweo.
Jana Maofisa wa wizara hiyo walikamata samaki aina ya sato (wasiofikia kiwango cha kuvuliwa) kiasi cha kilo mbili kati ya 100 waliokuwa wakiuzwa kinyume cha sheria katika mgahawa wa ofisi ya Bunge ambapo walikuwa wakipima urefu wa samaki kwa kutumia rula ya daftari.
Baada ya hapo, mmiliki wa mgahawa huo, Daniel Lamba, alipigwa faini ya Sh. 300,000 baada ya kukiri kosa la kukutwa na samaki hao wachanga.
John Mpepele ambaye ni Msemaji wa wizara hiyo alisema walipata taarifa za kuwepo samaki hao kutoka kwa Waziri wa Wizara hiyo, Luhaga Mpina aliyekuja kwenye mgahawa huo juzi asubuhi.
Comments are closed.