Waziri Awachukulia Hatua Wasanii Wanaovaa ‘Kihasara’ (Video)
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, amesema serikali inafuatilia kwa karibu wasanii wote wanaoweka picha zisizo na maadili kwenye mitandao na itawachukulia hatua.
Shonza ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaama alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari akisisitiza agizo lililotolewa na Rais John Magufuli mjini Dodoma wakati akizungumza na Jumuiya ya Wazazi ya CCM ambapo alivitaka vyombo husika kuwachukulia hatua wasanii hasa wa kike ambao wamekuwa wakivaa nguo zinazosababisha kumomonyoka kwa maadili.
Shonza aliwataja kwa majina wasanii ambao wameanza kuwachukulia hatua ambapo baadhi wametakiwa kufika ofisini kwake ambapo mmoja amefungiwa kujihusisha na masuala ya sanaa kwa muda wa miezi sita.
Shonza amemtaka msanii, Jane Rimoy maarufu kwa jina la Sanchi kufika ofisini kwake mara moja kutokana na kuchapisha mitandaoni picha zisizo na maadili.
Mbali na Sanchi, waziri amesema: “Ninamtaka Msanii wa Bongo Fleva, Gift Stanford maarufu kama Gigy Money kufika ofisini kwangu mara moja sababu alitumiwa ujumbe lakini hakujibu, hivyo ajue kuwa hawezi kushindana na serikali.”
Pia, amemfungia msanii wa filamu na muziki, Suzan Michael maarufu Pretty Kind, kujihusisha na shughuli zote za sanaa kwa muda wa miezi sita, kutokana na kuweka picha za utupu katika mtandao ya kijamii.
Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, amewasisitiza wamiliki wa studio za kutayarisha kazi za sanaa na waandaji wa kazi za sanaa (Producers) kujisajili katika ofisi za baraza hilo akisisitiza kufanya kazi bila kusajiliwa ni kinyume na sheria.
Comments are closed.