The House of Favourite Newspapers

Waziri Aweso Afanya Ziara ya Kikazi Italia

0

Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amefanya ziara ya kikazi Rome-Italy hivi karibu mwezi Mei mwaka 2023 na kupokelewa na mwenyeji wake Balozi wa Tanzania nchini Italia,  Mahamood Kombo.

Katika ziara hiyo, Aweso alipata fursa ya kushiriki mikutano mbalimbali ya kimkakati kwa lengo la kuvutia uwekezaji na kukuza mashirikiano kutoka kwa taasisi na makampuni ya Italia ili kuja kuwekeza katika sekta ya Maji hapa nchini.

 

Katika kikao cha kwanza alikutana na viongozi wa Shirika la SACE ambalo ni Shirika la Maendeleo la Italia kwaajili ya  Maendeleo ya Viwanda.

Aidha, pamoja na mambo mengine shirika hilo linajishughulisha na ukuzaji wa tekenelojia mbalimbali ya kuendeleza viwanda katika nchi mbalimbali duniani. Katika kikao hicho Mheshimiwa Waziri Aweso alieleza fursa za uwekezaji  zilizopo katika  sekta ya maji hapa nchini na kuwasihi kuja kuwekeza na kuleta teknolojia mpya itakayo saidia kuendeleza sekta ya maji.

 

Kiongozi wa shirika hilo walivutiwa na fursa zilizopo kwenye sekta ya maji na walionesha nia kuja na kufanya mazungumzo ya kina na watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji ili kuendeleza uwekezaji katika sekta ya maji.

Aidha, Mheshimiwa Aweso alipata fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Benki ya Maendeleo ya Italia (CDP) na alielezea mipango ya sekta ya maji na miradi ya kimkakati inayohitaji kutekezwa kwa ubia  kati ya  Serikali na sekta binafsi (PPP).

 

Vilevile, alielezea kuhusu miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi  hapa nchini iliyofanyiwa tathimini ya kina na Benki hiyo na kuisihi  Banki ya Maendeleo ya Italia (CDP) kuendelea kushirikana na Serikali  ya Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabiachi ambayo yamekuwa na athari katika sekta ya maji.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Aweso alitembelea baadhi ya Viwanda vinavyozalisha vipuri mbalimbali ikiwa ni pamoja na pampu za maji  na mabomba ya maji na kuona teknolojia ya kisasa inayotumika katika uzalishaji wa vifaa hivyo na aliwasihi pamoja na kuwakaribisha viongzoi wa viwanda hivyo kuja kuwekeza Tanzania ambapo mahitaji ya uwekezaji wa aina hiyo ni mkubwa na itasaidia Tanzania kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maji kwa gharama nafuu.

Ziara ya Mheshimiwa Aweso ilihitimshwa kwa kikao kazi Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchini Italia ambayo ina dhamana ya  kuratibu Mikopo ya Kimataifa na Ufadhili kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha ya nchi hiyo ambapo Mheshimiwa Waziri Aweso alifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Wizara ya Mambo Nje anaeshughulika masuala ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Balozi Giussepe Mistretta ambaye alishiriki kwaniaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia.

Leave A Reply