Waziri Junior Avunja Mkataba Yanga Awaaga Mashabiki

MSHAMBULIAJI Mpya wa Yanga SC, Waziri Junior amevunja mkataba na klabu yake Yanga kwa kuununua, mara baada ya kujiunga nao msimu uliopita akitokea Mbao FC ya Mwanza.

Waziri amechukua uamuzi huo akiamini anahitaji kujaribu nafasi yake sehemu nyingine. Tayari amepokea ofa ndani na nje ya nchi.

Waziri Junior kwa sasa ni mchezaji huru (Free Agent). Wakala wake Ismail Mwakabwangas @ismailxm amethibitisha hilo.

Kupitia page yake ya Instagram Waziri Junior amewaaga wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu hiyo.

“Nichukue fursa hii kuwashukuru sana wana Yanga kuanzia makocha, wachezaji, viongozi na mashabiki kwa kuniamini na kuwa mmoja wao. Haikuwa safari rahisi licha ya kuwa fupi mno.

 

Nilifika Yanga SC nikiwa na malengo makubwa lakini haikwenda kama nilivyotarajia labda kwa sababu zangu binafsi au vinginevyo. Ni kawaida yetu sisi wanasoka kukutana na changamoto kama hizi.

 

Nimechukua maumuzi mgumu sana kwangu lakini yote ni kwa maslahi mapana ya ufanisi wangu. Nimeona nihamishie jitihada zangu sehemu nyingine.

 

Yamkini sikufikia malengo ya klabu na kutokuwapa mashabiki ile furaha waliyotarajia kutoka kwangu lakini niwatoe shaka kuwa haikuwa dhamira yangu kuwaangusha.

 

Niwatakie kila la kheri kwenye safari yenu kuelekea msimu ujao. Tuendelee kuombeana labda ipo siku tutakuwa pamoja tena kama sio, basi nitaendelea kuuenzi upendo na imani mliyoijenga kwangu. Najivunia kuvaa nembo ya Klabu Kubwa hapa nchini. Asante (mungu kwanza). ” alisema Waziri Junior @wazir_junior_10.

 


Toa comment