The House of Favourite Newspapers

Waziri Lukuvi asitisha zoezi la bomoa bomoa Dar

0

lukuviWaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nchini, Mhe. William Lukuvi.

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesimamisha kazi ya bomoabomoa kwa siku 15 kwa wavamizi waliojenga katika Bonde la Mto Msimbazi, Dar es Salaam na kuwataka wavamizi hao kubomoa wenyewe na kuondoka maeneo hayo, kabla ya kazi hiyo kuanza tena Januari 5, mwakani.

Aidha, wale wote waliojenga kwenye maeneo ya wazi, wavamizi wa maeneo ya watu, maeneo ya shughuli za kijamii kwenye fukwe, kingo za mito na vyanzo vya maji nchi nzima, kazi ya ubomoaji itaanza mapema Januari mwakani na kwamba hakuna atakayefidiwa.

Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Waziri wa Wizara hiyo, William Lukuvi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, wakati wakizungumza na waandishi wa habari.

Lukuvi alisema wameamua kusimamisha kwa muda kazi hiyo ili kutoa nafasi kwa wavamizi hao kubomoa wenyewe nyumba walizojenga kinyume cha sheria ili waambulie vitu vyao na baada ya muda uliotolewa kumalizika, kazi ya ubomoaji itaendelea na hakuna atakayelipwa fidia.

Alisema katika eneo hilo la Bonde la Mto Msimbazi, nyumba 8,000 zimejengwa isivyo halali na hadi sasa nyumba 395, zimebomolewa kwa siku tatu kuanzia Desemba 17 na kwamba wavamizi hao wasitegemee kulipwa fidia.

“Hakuna fidia kwa wavamizi hao, kama huku nyuma kuna watu walionewa huruma kwa sababu ya maafa na kupewa viwanja, ilikuwa ni huruma tu, hakuna sheria inayomruhusu mtu kujenga kwenye eneo hatarishi, hivyo tutakuondoa tu na hakuna fidia,” alifafanua Lukuvi.

Alisema hakuna nyaraka zilizotolewa kwa wavamizi hao kujenga maeneo hayo, na kama kuna mtu ana kibali cha ujenzi kwenye eneo hilo hatarishi au kingo za mto, sheria ya mazingira itamuondoa na hakuna watakaoachwa.

Kwa upande wake, January alisema Sheria ya Mazingira iko wazi na inakataza watu kufanya shughuli kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa sababu za kulinda mazingira na vyanzo vya maji.

Alisema kuanzia mwakani, wizara hiyo itaendesha operesheni ya kuwaondoa watu wanaoishi na kufanya shughuli kwenye maeneo ya kingo za mito na maziwa, fukwe za bahari, maeneo oevu na maeneo ya wazi. Kwa Dar es Salaam, maeneo ya wazi 180 yamevamiwa, kati ya hayo 111 yapo Halmashauri ya Kinondoni, 50 yapo Ilala na Temeke yapo 19.

Leave A Reply