



WAZIRI wa Ardhi Nyumba Maendeleo na Makazi ,William Lukuvi, amezitaka Taasisi za Kifedha hapa nchini ikiwemo Benki kuwawezesha wananchi wa hali ya chini kupata mikopo ya nyumba kwa riba nafuu.
Aidha amezitaka taasisi hizo za kifedha kushirikiana na kampuni za ujenzi ili kuwasaidia wananchi wanaochukua mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, kumiliki nyumba kwa gharama nafuu.
Waziri Lukuvi aliyasema hayo jijini Arusha katika maonyesho ya NMB Nyumba Day, yaliyofanyika jijini hapa na kukutanisha wateja na watoa huduma katika ujenzi na uuzaji wa nyumba ambapo Benki ya NMB inatoa huduma ya mikopo kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kumiliki nyumba.
Amesema kuwa taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya nyumba zinatakiwa kutafuta namna ya kuwasaidia wananchi ili kuweza kumudu na kupata nyumba kwa gharama nafuu.
“Ili gharama za ujenzi wa nyumba za Tanzania zisiwe za ghali taasisi za kifedha kuweni na mpango mahsusi, endelevu na ulio rahisi wa kumkopesha mtu nyumba,ili wananchi wa hali ya chini kupata mikopo kwa riba nafuu na mshirikiane na kampuni za ujenzi ili kuwasaidia wananchi wanaochukua mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba,kumiliki nyumba kwa gharama nafuu,” alisema.
Waziri Lukuvi aliipongeza Benki ya NMB kwa kuanzisha mikopo hiyo ambapo ni miongoni mwa Benki zilizopo hapa nchini ambazo zinashirikiana na wadau wengine kuhakikisha wananchi wanapata mikopo kwa riba nafuu na kuwawezesha kumiliki nyumba za makazi.
Awali Kaimu Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati kutoka Benki ya NMB, Salie Mlay,anasema benki hiyo imekuwa baina ya wananchi na serikali katika kuwawezesha wananchi ili wapate makazi bora.
Anasema kupitia mikopo hiyo wanawawezesha hata waliojenga nyumba na kushindwa kuzimalizia na kutaja mikopo mingine wanayoitoa ni kwa wale waliojenga nyumba zao na kuzimaliza ambao wanataka kujenga nyumba nyingine na kuwa katika mikopo hiyo wanatoa asilimia 80 ya thamani aliyojengea nyumba iliyokamilika.
Anasema mikopo hiyo ilianza miaka miwili na hadi sasa wameshatoa mikopo ya Sh Bilioni 17 kwa wateja 139 na kuwa mikopo hiyo hutolewa kati ya Sh Milioni 10 hadi Sh Milioni 700.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi walioshiriki maonyesho hayo walishukuru Benki hiyo kwa elimu pamoja na fursa hiyo ya mikopo ya nyumba ambayo itawawezesha kupata mikopo ya nyumba.
“Nimefurahia kupata elimu hii ya mikopo ya kuwezeshwa kujenga nyumba,tumefunguka kwani wengi tulikuwa hatuelewi hivi sasa najua nikitafuta hati miliki ya eneo langu naweza kuitumia kuomba mkopo na kujenga nyumba,”anasema mmoja wa wananchi hao, Adelvina Ngalo


Comments are closed.