Lukuvi: Wadaiwa Kodi ya Ardhi Walipe Kabla ya Juni 20, 2019 – Video

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi wanatakiwa kulipa kodi hiyo kabla ya Juni 20 na mwisho wa zoezi la kulipa madeni hayo ni Novemba ili kuepuka hatua za kisheria zitakazochukuliwa ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali husika.

 

Ameyasema hayo leo jijini Dodoma ukumbi wa Hazina alipokuwa akiongea na wawakilishi wa taasisi mbalimbali wanaodaiwa kodi ya pango.

 

“Baada ya muda uliotajwa kwisha wadaiwa watakaoshindwa kulipa kodi hatua za kisheria zitafuata ikiwa ni pamoja na kunadi mali na kuuza viwanja husika, taratibu hizi za kisheria zitachukuliwa ili kulipa kodi na malimbikizo yanayodaiwa.

 

“Msingi wa shughuli na biashara zote mnazofanya ni ardhi lakini hakuna anayejituma kulipa kwa hiari na wengine wananiandikia barua kuomba kufutiwa au kupunguziwa kodi lakini sijawahi kuona hata mmoja kati yenu anaomba kufutiwa bili ya maji au umeme,” alisema na kuongeza:

 

“Kama unataka usiwe unalipa kodi kubwa kila mwaka hakikisha unalipa kwa wakati ili malipo yako yasiambatane na riba, hivyo jitahidi ukifika mwezi Julai unalipa kodi zako ili kuepuka malimbikizo.

 

Alisema kwamba kulingana na tangazo lake la Julai 2018 kuna dhana potofu juu ya msamaha wa kodi ya pango ya ardhi kwa taasisi na mashirika ya umma yanayotoa huduma kwa jamii,  na kwamba tangazo hilo limefafanuliwa kwa kina katika Marekebisho ya Sheria ya Ardhi Sura 113.

 

Akisisitiza, alisema taratibu zilizowekwa kwenye kanuni za msamaha zinawataka wahusika kuandika barua ya kuomba kupatiwa msamaha kwa kuzingatia vigezo ikiwemo kueleza kama ardhi husika haitumiki kibiashara.

 

“Hadi sasa wizara yangu haijapokea maombi yoyote kutoka kwenu kuonyesha kwamba hamtumii ardhi kibishara.  Huwezi kuwa unapokea ada ya wanafunzi halafu useme hufanyi biashara, tunajua tukienda makanisani hatutozwi fedha.  Hao wanaweza wakalalamika,” alisema Lukuvi.

Baadhi ya Taasisi za Serikali zinazodaiwa kodi ya Ardhi na zimepewa siku 9 kulipa kati ya taasisi 207 zinazodaiwa billion 200 :

Kampuni ya Simu ya TTCL Bilioni 40.1

Shirika la umeme TANESCO Blioni 25.5

Ranchi za taifa NARCO 23.4

Benki ya NBC Bilioni 17.5

Chuo kikuu cha Sokoine SUA Bilioni 10.7

Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Bilion 9.19

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege TIA bilioni 8.14

 

Taasisi ya Elimu ya Kibaha Bilioni 5.5

SIDO Bilioni 3.7

NHC Bilion 3 .4

VETA Bilion 3.2

Chuo kikuu cha Dar es Salam Bilion 2.3

 


Loading...

Toa comment