Waziri Mchengerwa Akemea Wanasiasa Wanaokwamisha Miradi Ya Maendeleo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed Mchengerwa amekemea tabia ya wanasiasa na watumishi wa serikali kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema wakati wa uongozi wake watu wa aina hiyo atawashughulikia bila kuwamuonea haya.
Mchengerwa ameyasema hayo mjini Bukoba wakati wa hafla ya utiliaji Saini mikata ya usanifu wa miradi ya uboreshaji miundombinu ya miji Tanzania (TACTIC) kwa ajili ya miji 15 ya kundi la pili (Tier2) ambayo utekelezaji wake utagharimu Sh bilioni 8.25.
Amesema taarifa alizonazo ni kuwa, kumekuwapo na baadhi ya wanasiasa ambao kwa maslahi yao binafsi na ya kisiasa wamekuwa wakikwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Bukoba na maeneo mengine mkoani Kagera.
“Ninatambua wako baadhi ya wanasiasa wanaojali matumbo yao ambao wanaokwamisha kwa makusudi utekelezaji wa miradi hivyo sitowavumilia kwani wanakwamisha jitihada za Rais za kuleta maendeleo”. amesisitiza.
Amesema wapo baadhi ya madiwani wanakwamisha miradi ya maendeleo katika Manispaa ya Bukoba na kuonya kuwa hatasita kusitisha vikao vya Baraza la Madiwani katika Manispaa ya Bukopa mpaka watakapokamilisha miradi.
“Kiongozi yeyote wa kisiasa anayepanga kukwamisha utekelezaji wa miradi hii ambayo Mhe. Rais Dkt. Samia ameamua kuwakomboa wana Bukoba kiongozi huyo nitamshughulikia ipasavyo,”
Amesema Mkoa wa Kagera unachelewa kupata maendeleo kwasababu kuna baadhi ya watu wanauhujumu kwa kujali maslahi yao binafsi hususani ya kisiasa.
Ameongeza kuwa, kuna baadhi ya maeneo miradi haitekelezwi vizuri kwasababu baadhi ya viongozi wa Serikali wanaingilia mchakato wa zabuni na kuzipatia kampuni zao.
Awali, akitoa maelezo ya mradi wa TACTIC, Mratibu wa Kikundikazi kinachosimamia miradi inayopata fedha kutoka Benki ya Dunia Bw. Humphrey Kanyenye, alisema mradi unagharamiwa na serikali kuu kwa Shilingi trilioni moja kupitia masharti ya nafuu ya mkopo kutoka Benki ya Dunia na utanufaisha Miji 45.
“Mradi utatekelezwa kwa miaka sita kuanzia mwaka wa fedha 2022/23, lengo kuu ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa miji.