The House of Favourite Newspapers

WAZIRI MGUMBA AWATAKA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA KWENYE KILIMO

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba akizungumza katika uzinduzi wa Jukwaa la Vijana wa Mkoa wa Morogoro jana Machi 23, 2019.
Meza kuu ilivyoonekana wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana wa Mkoa wa Morogoro.

 

 

 

VIJANA Mkoani Morogoro wametakiwa kuchangamkia fursa za kilimo zilizopo katika Mkoa huo ili kujiwezesha na kujiimarisha kiuchumi.

 

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba jana Machi 23, mwaka huu wakati akizungumza katika uzinduzi wa Jukwaa la Vijana wa Mkoa wa Morogoro kwenye mkutano ulioudhuriwa na Vijana wa Mkoa huo pamoja viongozi mbalimbali.

 

 

Naibu waziri Mgumba amewataka Vijana hao kuchangamkia fursa hizo ikiwa ni pamoja na kupata mkopo kutoka  Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na mikopo ya Matrekta kutoka Shirika la maendelo la Taifa (NDC) Mjini Kibaha ili kuweza kujiari katika sekta hiyo.

 

 

Amesema kuwa Mkoa wa Morogoro umepata bahati ya kuwa na viwanda vikubwa ambavyo vinahusika katika sekta ya Kilimo ikiwemo Kiwanda cha  Mtibwa, kilombero, Mkulazi 1 na 2, Mansoor industry cha kutengeza Sigara, ujenzi wa Kiwanda cha kukoboa Mpunga na Kiwanda cha kuchakata  mazao ya jamii ya Mikunde cha Maharage.

 

Mgumba amewataka Vijana kutosubiri ajira za kuajiwa ofisini na badala yake waungane kwa pamoja kwa kuanzisha mashamba, kushiriki katika ujasiriamali wa mazao ya kilimo, kutoa huduma kwenye sekta ya kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ili kutengeneza ajira.

 

 

Akizungumza na mamia ya Vijana wa Mkoa wa Morogoro katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Waislamu mkoani Morogoro Naibu waziri Mgumba amewahakikishia Vijana kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuwakomboa wakulima kupitia mazao ya Kimkakati kupitia Programu kabambe ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili yaani ASDP II.

 

Alisema kuwa ni vyema Vijana hao wakashirikiana na wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha wanalima Kilimo chenye tija, na kujiunga kwenye Vikundi na kuwa na ardhi zenye hati miliki zitakazo tumika kwa ajili ya uzalishaji mali na kuwa dhamana kwenye taasisi za fedha kupata mitaji ya kuwekeza kwenye kilimo.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe amesema kuwa Mkoa huo umebarikiwa kwa kiasi kikubwa kwani asilimia kubwa ya mazao mbalimbali hustawi vizuri.

 

 

Dkt Kebwe amesema kuwa Mkoa huo pia una ardhi kubwa ambayo inafaa kwa Kilimo ikiwemo cha umwagiliaji kutokana na kuwepo na mito mingi ambayo itamuwezesha mkulima kulima kwa kipindi chote.

Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwapongeza Vijana wanaohitimu chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa jitihada zao za kujiingiza katika Kilimo na kutosubiri ajira za serikali.

 

 

Jukwaa la Vijana Mkoa wa Morogoro limezinduliwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Suleiman Jafo ambapo amewataka Vijana hao kuhakisha wanatumia vyuo vya Kilimo vilivyopo katika Mkoa huo kubadilisha hali ya Mkulima.

 

Jukwaa la Vijana Mkoa wa Morogoro limezinduliwa likiwa na kauli mbiu “Fursa Zetu Mkoa Wetu”

 

 

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Comments are closed.