Kuanzia sasa serikali itaanza kuzitazama ajira za vyuo vikuu badala ya kuangalia ubora wa ufaulu yaani GPA pekee sasa waajiriwe kwa kupimwa uwezo wao kwa kufanya usaili.
Kuangalia ufaulu pekee wa wanafunzi haitoshi kuboresha elimu badala yake ni muhimu kuongeza vigezo hivyo katika mapitio ya sera na mabadili ya mitaala jambo hilo litatazamwa kwa weledi mkubwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 12 Disemba 2022 mbele ya mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Mpango wakati wa mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania iliyofanyika Kinondoni Jijini Dar es salam.
Amesema wakati serikali inaongeza udahili wa wanafunzi haitakuwa tayari kuona ubora unapungua hivyo serikali inaendelea na mkakati wake wa kuhakikisha ubora wa elimu hususani katika vyuo vikuu unaimarika.
“Zamani ilikuwa rahisi kuwa Profesa ukiandika tu kwenye magazeti unakuwa Profesa lakini kwa sasa vigezo vya kuwa Profesa vimezidi kuwa vigumu kwa sababu tunataka maprofesa wetu wawe sawa na wale wa nchi zingine” Amekaririwa Prof Mkenda
Amesema katika mageuzi ya elimu yanayokuja ambapo wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipo katika mapitio ya sera na mitaala miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa kazi itakuwa ni pamoja na kuhakikisha wanaoajiriwa ni wanafunzi wenye sifa zinazotakiwa.
Pia, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali kwa sasa inaendelea na Ujenzi wa Kampasi mpya za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 Tanzania pamoja na upande wa Zanzibar (Unguja na Pemba) katika maeneo ambayo hayana vyuo vikuu ukiacha vyuo huria.
Mikoa hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na kampasi za vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini ni pamoja na Tabora, Katavi, Kigoma, Kagera, Singida, Manyara, Lindi, Rukwa, Mwanza, Simiyu, Tanga, Ruvuma, Shinyanga na Dodoma.
Kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa hapa nchini karibu kila mkoa una kampasi ya chuo kikuu huria cha Tanzania hivyo ametoa rai kwa watanzania wengi kuitumia fursa hiyo.
Kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali imejipanga kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi lakini mikopo yote itatolewa kwa haki na vigezo vilivyowekwa.
“Hakuna kitu kibaya kama kuachia madaraka makubwa kwamba aniletee kimemo mimi nimuangalie mtoto fulani ndio nimsaidie kupata mkopo wakati muhusika mwenyewe anaweza akamsomesha mwanae, wakati mkopo wenyewe hautoshi, mimi ningependa tuwape wenye mahitaji makubwa zaidi”
“Mtu yeyote anayefanya kosa la kumnyima yatima fursa ya kusoma kwa sababu tu ya kujipendekeza kumpa mtoto wa fulani mkopo huyo nadhani atalaaniwa vilevile” Ameseisitiza Waziri Mkenda
Waziri huyo wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amemuhakikishia mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Philip Mpango kuwa ataendelea kusimamia utoaji wa mikopo bila kutetereka ili kuwe na uwazi na utoaji wa mikopo kwa haki.
Na Mathias Canal, WEST-Dar es salaam