Waziri Mkuu Azitaka Taasisi za Umma na Binafsi Kuacha Kutumia Kuni na Mkaa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezitaka Taasisi za Umma na Binafsi zinazo andaa chakula kwa watu zaidi ya 100 kuacha matumizi ya kuni na mkaa badala yake kuanza kutumia teknolojia ya nishati safi ya kupikia, huku akitoa ukomo wa mwezi wa 12 mwaka huu kuwa ndio mwisho wa kutumia mkaa na kuni kwa Taasisi hizo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali itafanya ukaguzi kwa kila Taasisi kuona utekelezaji wa agizo hilo.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Novemba 07, 2024 alipotembelea na kukagua hatua za maandalizi ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi za kupikia katika Gereza la Isanga, Dodoma na kusisitiza kuwa mkakati huo unalenga Magereza yote na vyuo vya mafunzo ya kijeshi nchini nzima, na Taasisi zote za elimu za bweni nchini.
Sambamba na hilo Waziri Mkuu amebainisha manufaa ya kutumia nishati safi ya ikiwemo kutokuwepo na moshi wakati wa utumiaji hivyo kupunguza madhara ya kiafya kwa mtumiaji tofauti na matumizi ya kuni pia teknolojia hiyo inauwezo wa kupika chakula kingi kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameishukuru Serikali kwa kazi inayofanya katika kuleta mabadiliko makubwa kwa Wizara na vyombo vyake vya usalama ikiwemo Jeshi la Magereza.
Mhandisi Masauni amesema Gereza hilo la Isanga limechangamkia fursa ya utekelezaji wa azma ya Serikali kwa vitendo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa nishati safi za kupikia Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Jeremiah Katungu amesema Gereza hilo limeshaanza utekelezaji wa mkakati huo kama ilivyokusudiwa kwa kupokea jumla ya tani 15 za mkaa mbadala na majiko sita na utaratibu wa kusimika mifumo ya matumizi ya gesi ya LPG unaendelea na utakamilika hivi karibuni.