The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa awakomesha mastaa

0

MAJALIWAPMWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa

STORI: MWANDISHI WETU, AMANI

DAR ES SALAAM: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewakomesha baadhi ya mastaa wa kada mbalimbali Bongo baada ya kuvitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaojihusisha na ishu ya biashara ya kilevi cha shisha ambacho hutumiwa na mastaa wengi Bongo.

Muda mfupi baada ya tamko hilo lililotolewa na Waziri Mkuu Majaliwa jijini Dar kwenye hafla ya kufuturisha iliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) na waumini wa Dhehebu la Shia, baadhi ya mashabiki wa mastaa hao walifurahishwa na kitendo hicho kwani shisha imekuwa kilevi kikuu kwa baadhi ya mastaa hao.

Tamko la Majaliwa lilikuja siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda kutoa siku saba kwa wanaojihusisha ishu hiyo kuacha mara moja kabla ya vyombo vya sheria kuwachukulia hatua.

“Kiukweli Waziri Mkuu na Makonda wamewakomesha mastaa maana tulizoea kuwaona wakijazana pale Coco (Beach), Kinondoni na Sinza kwenye Baa za Barabara ya Shekilango kwa ajili ya kuvuta shisha lakini tangu tamko hilo limetoka hawaonekani.

“Kwanza kuna wengine huwa wanatumia kwa siri lakini hata wao wamekomeshwa.

“Hata mastaa wa nje kama Ne-Yo wa Marekani ambaye aliwahi kuripotiwa kuvuta shisha akiwa na Ali Kiba (msanii wa Bongo) huko nchini Kenya, nao wakija Bongo watakuwa hawapati ulevi huo,” alisema mmoja wa wasanii ambaye yeye alidai kuwa hatumii kilevi hicho.

Mbali na mastaa hao, baadhi ya warembo na watoto wa mjini nao wamekomeshwa kwani wamekuwa wateja wakuu wa shisha jijini Dar.

Shisha ambayo uchunguzi wa gazeti hili unaonesha kuwa imepanda bei baada ya kupigwa marufuku, huwa ni mchanganyiko wa tumbaku au bangi, moto, maji na vitu ambavyo hutoa harufu nzuri za kuvutia huku ikiwa na madhara kwenye mwili wa binadamu kama kusababisha kansa ya mapafu na kifua kikuu.

Leave A Reply