Waziri Mkuu: Ma-RC anzisheni vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kabla ya 2024
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini ambao bado hawajaanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 wawe wameshaanzisha kabla ya mwaka 2024.
Pia, Majaliwa amewataka Viongozi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na Sekta Binafsi waimarishe huduma za uwezeshaji ili waweze kuyafikia malengo waliojiwekea na kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uwezeshaji na kupunguza umaskini nchini.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Jumatatu, Oktoba 2, 2023 wakati akifunga Kongamano la Saba la Uwezeshaji Kiuchumi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. “Suala la kuanzisha vituo vya uwezeshaji ni maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 katika Ibara ya 26 (k) na hili ni jukumu letu viongozi kuhakiksha ilani inatekelezwa.”