The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu Majaliwa Azindua Kampeni ya Mama Samia, Atembelea Banda la NMB

0
Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa (kulia) akimsikiliza Mkuu wa Idara ya Biashara za Serikali wa Benki ya NMB, Vicky Bishubo ( kushoto) alipotembelea banda la benki hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya “Mama Samia legal Aid” yenye lengo la kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi hususani walio maeneo ya pembezoni. Wapili kulia ni Waziri wa Katiba na sheria, Dkt. Damas Ndumbaro na wengine ni watumishi wa Benki ya NMB
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka watanzania kuitumia kampeni ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu au vikundi vya watu ambao wanajihusisha na ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto.
Majaliwa alitoa wito huo Alhamisi tarehe 27 Aprili 2023 alipozindua kampeni hiyo ambayo itatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia Machi, 2023 hadi Desemba 2025.
Katika uzinduzi huo, Majaliwa alitembelea mabanda mbalimbali ikiwemo la Benki ya NMB na kuzungumza na wafanyakazi wa benki hiyo akiwemo, Mkuu wa Idara ya Biashara za Serikali wa Benki Ya NMB, Vicky Bishubo.
Majaliwa alisema kampeni hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa sheria na upatikanaji haki, mifumo ya utoaji haki, masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa kushirikiana na taasisi za serikali, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi.
“Kampeni hii pia itasaidia kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususani wanawake, watoto na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu. Vilevile, itachangia kuimarisha amani na utulivu, kuongeza kipato cha mmoja mmoja na kuleta utengamano wa kitaifa,” alisema
Aliongeza faida nyingine ya kampeni hiyo ni kusaidia kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi zote yaani kuanzia Serikali kuu hadi Serikali za Mitaa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Katiba na Sheria iweke mfumo mzuri wa kushughulikia changamoto za kisheria zitakazoibuliwa wakati wa Kampeni katika utimilifu wake.
“Tusiache wananchi wakiwa bado hawajapata majibu ya changamoto zao. Hii itasaidia kujenga taswira nzuri kwa Serikali wala kwa mamlaka ambayo imeridhia kuwepo kwa Kampeni hii,” alisema
Kadhalika, Majaliwa ameitaka Wizara hiyo itekeleze majukumu yake kwa ufanisi na weledi mkubwa ili Watanzania wote waweze kuifikia haki na kuipata haki  kwa wakati.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro alisema kampeni hiyo ambayo ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanatoa elimu ya sheria na kusaidia wahitaji ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, wamepanga kutoa elimu katika maeneo ya migogoro ya Ardhi, mirathi, ndoa, sheria ya mtoto katika maeneo ya Ukatili wa kijinsia na Maadili.
Alisema kampeni hiyo itatekelezwa pande zote mbili za Muungano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali na wasio wa serikali ikiwemo Ofisi ya Mashtaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ustawi wa Jamii, vyuo vya elimu ya juu.
Leave A Reply