The House of Favourite Newspapers

Waziri Mkuu Majaliwa, Mgeni Rasmi Pambano la Mandonga na Mbelwa, Ruangwa

Mandonga Aja na Ngumi Mpya

Promota wa pambano hilo, Evarist Ernest (katikati) akiwainua mikono mabondia, Karim Mandonga (kushoto) na Said Mbelwa kwenye mkutano na wanahabari leo.

Dar es Salaam 14 Machi 2025: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye pambano la Bondia mwenye mbwembwe nyingi, Karim Mandonga na Saidi Mbelwa ambalo linatarajiwa kufanyika Ruangwa mkoani Lindi, siku ya iddi pili.

Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam leo promota wa pambano hilo, Evarist Ernest maarufu kama Mopao ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapromota amesema maandalizi yote ya pambano hilo yameshakamilika na kinasubiriwa ni siku na saa.

Mopao amesema katika pambano hilo lisilo la ubingwa litatanguliwa na mapambano kumi yakihusisha mabondia kutoka Dar, Masasi, Nachingwea na Ruangwa.

Wakiwa kwenye mkutano na wanahabari leo bondia hao kila mmoja alimwaga tambo za kummaliza mwenzake na kumkata ngebe mapema huku mandonga kama kawaida yake sasa hivi amejitapa kuja na ngumi yake mpya iitwayo ‘Kaniki’ ambayo amesema kwa mganga ipo na kwa mchawi ipo. HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN /GPL