Waziri Mkuu Mstaafu Pinda Afurahishwa na Ilipofikia VETA

Dar es Salaam, 20 Machi 2025: Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda, leo ametembelea kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 30 ya VETA linaloendelea kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere JNICC Jijini Dar, na kuonesha kufurahishwa na aliyojionea.
Waziri Mkuu Mstaafu Pinda alifika kwenye kongamano la maadhimisho hayo na kujionea mambo mbalimbali ya kiteknolojia ikiwemo mifumo ya umeme, uchongaji, uhandisi majengo, mifumo ya maji, ushonaji, ufundi vyuma, useremala, upishi, ushonaji kilimo, ufugaji na mengineyo.

Baada ya kujionea mambo mbalimbali ya kibunifu kwenye mabanda ya maonesho Pinda aliisifu VETA ilipofikia na kusema kama tukiendelea hivi na kujiboresha zaidi kiteknolojia basi tutafika mbali na itakuwa ndiyo ukumbozi wa taifa letu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore amemshukuru Waziri Mkuu Pinda kwa kuweza kufika kwenye kongamano hilo na kujionea kinachoendelea VETA.

CPA Kasore amesema si kwamba, Waziri Mkuu Mstaafu Pinda ni mgeni VETA bali amefika kwenye kongamano kujionea ilipofikia maana akiwa Waziri Mkuu alihusika kusimamia maboresho makubwa yaliyoifikisha VETA hapa ilipofikia. HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN /GPL